Viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wametakiwa kujenga tabia ya kuhudhuria vikao na mikutano ya chama hicho kwa lengo la kukiimarisha zaidi kisiasa na kuendelea kuleta maendeleo kwa wananchi.
Wito huo ulitolewa na Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mawenzi, Mujibu Idrissa Abeid, mara baada ya kutangazwa kwa matokeo ya kura za maoni kwa nafasi ya udiwani zilizofanyika kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.
“Tumeshuhudia wanachama wengi wakijitokeza kupiga kura za maoni, wakiwemo viongozi wa mitaa na kata, huu ni ushahidi wa uimara wa CCM, ni muhimu sasa wingi huu ukaonekana pia kwenye vikao na mikutano mingine ya kimaendeleo,” alisema Abeid.
Abeid alisisitiza kuwa vikao hivyo ni jukwaa muhimu la kuunganisha mawazo ya wanachama na viongozi wa chama katika kupanga na kutekeleza shughuli za maendeleo zinazowanufaisha wananchi.
Akizungumzia hatua ya kura za maoni, Abeid alisema kuwa ni mwanzo wa safari ya kuelekea ushindi kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu, ambapo baada ya kupatikana kwa wagombea wa CCM na kudhibitishwa na vikao vya juu, kazi kubwa itakuwa kuwanadi kwa wananchi.
“Tutahakikisha tunanadi wagombea wetu kwa nguvu zote ili CCM ishinde na kuendelea kushika dola, ushindi huo utatuwezesha kutekeleza ilani ya uchaguzi ya mwaka 2025–2030 na kuleta maendeleo kwa wananchi,” aliongeza.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Kata ya Mawenzi ambaye pia alikuwa Mkurugenzi wa uchaguzi huo, Joanith John Byarushengo, aliwashukuru wajumbe kwa kushiriki kura za maoni kwa amani na utulivu, na kuwataka kuendeleza utulivu huo wakati wa uchaguzi mkuu.
Katika matokeo ya kura hizo za maoni, aliyekuwa Diwani wa Kata ya Mawenzi, Apaikunda Naburi, alipata ushindi kwa kura 58 kati ya kura 94 zilizopigwa, akiwashinda wapinzani wake wawili Saidi Sultan Mndeme aliyepata kura 29, na Abdi Mohamed aliyepata kura 6, kura moja iliharibika.












