MOSHI-KILIMANJARO.
Mgombea mwenza wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Emmanuel Nchimbi, anatarajiwa kufanya ziara ya kampeni ya siku mbili mkoani Kilimanjaro kuanzia Septemba 13 hadi 14, 2025.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo septemba 11,2025 na Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM mkoa wa Kilimanjaro, Abraham Urio, ziara hiyo itahusisha majimbo ya Hai, Siha, Vunjo, Moshi Mjini, Mwanga pamoja na Same Magharibi na Mashariki.
Urio alisema kuwa Septemba 13, Dk. Nchimbi ataanzia Wilaya ya Hai kabla ya kuelekea Siha (Sanya Juu) kwa ajili ya kuwasalimia wananchi na kunadi ilani ya chama hicho. Baada ya hapo, mchana atafanya mkutano mkubwa wa kampeni katika Jimbo la Vunjo, viwanja vya Polisi Himo, ambapo pia atazindua rasmi kampeni za mgombea ubunge wa jimbo hilo, Enock Koola.
Aidha, jioni ya siku hiyo, atahitimisha ratiba yake kwa kufanya mkutano wa hadhara katika viwanja vya Mashujaa, Moshi Mjini.
Kwa upande wa Septemba 14, Urio alisema Dk. Nchimbi ataanzia Mwanga Mjini kwa kusalimia wananchi na kunadi ilani ya uchaguzi, kisha ataelekea Same Mjini na baadaye kufunga ziara yake katika Jimbo la Same Mashariki.
“Tunawaalika wanachama na wananchi wote kuhudhuria mikutano hii kwa wingi ili kusikiliza sera na maelezo ya ilani ya CCM. Ilani hiyo imebeba mustakabali wa maendeleo ya wananchi kuanzia mwaka 2015 hadi 2030,” alisema Urio.

.jpg)