NJORO-MOSHI.
Mgombea Mbunge Mteule wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Bi. Esther Maleko, amewataka wanachama na wapenzi wa chama hicho kuungana kwa pamoja kuhakikisha CCM inapata ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Akizungumza Septemba 11,2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Reli, Kata ya Njoro, Manispaa ya Moshi, Maleko alisema ushindi wa CCM ni muhimu ili kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo iliyoanzishwa, ikiwemo ya miundombinu ya barabara, elimu na afya.
“Kazi yetu ni moja, kutafuta kura za CCM, tunapoomba kura kwa ajili ya Rais Samia pia tunaomba kura kwa wasaidizi wake, ili awe na watu wa kufanya nao kazi. Tumchague Ibrahim Shayo awe Mbunge wa Moshi Mjini na Mhandisi Zuberi Kidumo awe Diwani wa Kata ya Njoro,” alisema Maleko.
Aliongeza kuwa CCM imefanikiwa kutekeleza kwa ufanisi mkubwa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020–2025, huku akieleza kuwa kazi kubwa zilizofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan zinaonekana wazi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Kwa upande wake, Mgombea Udiwani wa Kata ya Njoro kupitia CCM, Mhandisi Zuberi Kidumo, alisema kata hiyo imenufaika kwa kiasi kikubwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
“Tumeshuhudia maboresho makubwa kwenye miundombinu ya barabara, huduma za afya, elimu na hata michezo. Ujenzi wa wodi ya kisasa katika Zahanati ya Njoro umekamilika kwa msaada wa wadau, na vifaa vya matibabu vipo njiani kuwasili,” alisema Kidumo.
Aidha, alieleza kuwa kuna mipango ya kujenga wodi ya kina mama na mtoto, kuimarisha barabara za mitaa, pamoja na kuboresha masoko ya wananchi ili kuongeza kipato na kukuza uchumi wa kata hiyo.
"Njoro imekuwa mfano wa utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM, tutaendelea kusimamia utoaji wa mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani, ili makundi haya yaongeze kipato chao,” alibainisha.
Kidumo pia aliwataka wanachama wa CCM kuondoa tofauti zilizojitokeza wakati wa kura za maoni na kuungana kwa pamoja kuhakikisha ushindi wa wagombea wote wa chama hicho.
“Tunataka Njoro iwe kinara wa kura nyingi za CCM. Tukamchague Rais Samia, Mbunge Ibrahim Shayo na Diwani Zuberi Kidumo, ili tuendeleze miradi ya maendeleo na kuongeza ustawi wa wananchi wetu,” alihitimisha.
![]() |
![]() |
![]() |




















