KINDI-MOSHI.
Mgombea Ubunge wa jimbo la Moshi Vijijini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Morris Makoi, ametaja kipaumbele chake kikuu kuwa ni uboreshaji wa barabara, akisema kuwa ni msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa vijijini.
Akizungumza Septemba 12, 2025, mbele ya maelfu ya wananchi katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni zake uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Kindi, Makoi alieleza dhamira yake ya kuleta mageuzi katika sekta mbalimbali zikiwemo barabara, elimu, afya, maji, umeme, ajira kwa vijana na utawala bora.
![]() |
Aliahidi kuwa, iwapo atachaguliwa kuwa mbunge, atahakikisha barabara kuu zinazounganisha vijiji na kata zinajengwa kwa viwango vya kudumu kwa kushirikiana na TARURA na TANROADS Pia, alisema atawezesha ununuzi wa mitambo kama vile greda kwa ajili ya matengenezo ya barabara kwa kushirikiana na wananchi.
Makoi pia alimpongeza RaisSamiaSuluhuHassani, kwa kuendeleza miradi mikubwa ya maendeleo, na kuahidi kuunga mkono juhudi hizo kwa kuhakikisha Moshi Vijijini hairudi nyuma.
Kuhusu elimu, Makoi aliahidi kujenga na kukarabati shule za msingi na sekondari, kuhakikisha upatikanaji wa vitabu, vifaa vya maabara na kuhamasisha vijana kusoma masomo ya sayansi na ufundi ili kuwaandaa kuwa wataalamu wa baadae.
Katika sekta ya afya, alieleza kuwa atahakikisha vituo vya afya vinaongezwa na kuboreshwa kwa kuwa na vifaa tiba, dawa, wataalamu wa kutosha na magari ya kubebea wagonjwa, alisisitiza umuhimu wa huduma za afya kwa mama na mtoto, akiahidi kuwa akina mama wajawazito hawatapoteza tena muda kutafuta huduma kwa umbali mrefu.
Kuhusu upatikanaji wa maji, Makoi alisema miradi ya maji itasambazwa katika kila kata kwa kutumia vyanzo vya maji vya Mlima Kilimanjaro, teknolojia rahisi ya visima na mabwawa, kutegemeana na mazingira ya eneo husika.
Makoi aliahidi kuhakikisha vijiji na vitongoji vyote vinapata umeme kupitia Mradi wa REA pamoja na kuhimiza matumizi ya nishati jadidifu kama sola, alisema hatua hiyo itafungua fursa kwa viwanda vidogo, kusaidia shughuli za biashara na kuwezesha wanafunzi kusoma nyakati za usiku.
Katika eneo la uchumi, alisema atasimamia ipasavyo utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya halmashauri, inayopaswa kuwafikia wanawake (4%), vijana (4%) na watu wenye ulemavu (2%) kwa uwazi na bila upendeleo, ili kuwawezesha kuanzisha miradi ya maendeleo.
Makoi pia alieleza mikakati ya kuwainua vijana kupitia mafunzo ya stadi za kazi kupitia VETA na vyuo vya ufundi, pamoja na uanzishaji wa miradi ya kilimo, ufugaji wa kisasa na viwanda vidogo vya kuchakata mazao ya ndani kama kahawa, ndizi, maziwa na mifugo.
Akihitimisha hotuba yake aliyotumia muda wa dakika 16, Makoi aliahidi kusimamia utawala bora kwa kuhakikisha fedha za miradi zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, huku wananchi wakihusishwa katika kila hatua ya utekelezaji, viongozi wa vijiji na kata watapaswa kuwajibika moja kwa moja kwa wananchi.











