MOSHI-KILIMANJAO.
Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), kwa kushirikiana na taasisi binafsi ya TANLINK Health Care Foundation, imeanza kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na ongezeko la magonjwa ya moyo nchini, kwa kuzindua kampeni ya kuchangia ujenzi wa jengo maalum la matibabu na upasuaji wa moyo.
![]() |
| Dk. Siraj Mtulia, Mkurugenzi wa TANLINK Health Care Foundation |
Akizungumza Septemba 15, 2025 wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkurugenzi wa TANLINK Health Care Foundation, Dk. Siraj Mtulia, alisema kuwa duniani kote, magonjwa ya moyo husababisha si chini ya asilimia 32 ya vifo vyote, huku asilimia 75 ya vifo hivyo vikitokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati kama Tanzania.
"Takwimu zinaonyesha kuwa maradhi yasiyoambukiza, yakiwemo ya moyo, yanachangia takriban asilimia 30 ya vifo nchini. Hii ni changamoto kubwa inayohitaji hatua za haraka,” alisema Dk. Mtulia.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, zaidi ya shilingi bilioni 36 zinahitajika kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa mara baada ya kukamilika kwa jengo hilo, huku gharama za awali za ujenzi zikiwa bilioni 12. Wafadhili wameahidi kuchangia bilioni 10, na bado zaidi ya bilioni 3 zinahitajika kukamilisha mradi huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa KCMC, Prof. Gileard Masenga, alisema kukamilika kwa jengo hilo kutawarahisishia wananchi wa kanda ya Kaskazini kupata huduma za matababu ya moyo kwa gharama nafuu badala ya kusafiri kwenda hospitali nyingine kubwa ndani au nje ya nchi.
"Huduma zitakuwa karibu zaidi na wananchi, na hii itapunguza mzigo wa gharama kwa familia nyingi,” alisema Prof. Masenga.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, aliipongeza KCMC kwa ubunifu na jitihada za kuhakikisha huduma za moyo zinaboreshwa nchini.
“Magonjwa ya moyo ni tishio kubwa kwa maisha ya watu wetu. Kuwepo kwa kituo hiki kutasaidia wananchi kupata huduma bora bila kwenda mbali,” alisema Babu.
Aidha ktika uzinduzi huo jumla ya Sh milioni 30, zilipatikana huku ofisi ya mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro ikichangia kiasi cha Sh milioni 5.
Kampeni hiyo yenye Kauli mbiu " “KILA PIGO LA MOYO NI THAMANI, KILA UHAI NI MUHIMU”, inalenga kuhamasisha wananchi, mashirika, na wadau wa maendeleo kushiriki katika kuchangia ujenzi wa jengo hilo muhimu, ambalo linatarajiwa kuwa mkombozi kwa wagonjwa wa moyo katika Kanda ya Kaskazini na maeneo mengine ya Tanzania.
.jpg)














