DK. NGWARU MAGHEMBE; WANANCHI WA MWANGA WAZIDI KUIAMINI CCM, MIPANGO MIZURI YAENDELEA KUTEKELEZWA


MWANGA-KILIMANJARO .

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mwanga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ngwaru Maghembe, amesema kuwa wananchi wa Wilaya ya Mwanga wameendelea kuonyesha imani kubwa kwa chama hicho, hali inayoashiria uungwaji mkono wa dhati kwa sera na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Akizungumza leo septemba 14,2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya CD-Msuya, Dk. Maghembe alisema kuwa hata wananchi waliokuwa hawana imani na CCM hapo awali sasa wameanza kukikubali na kukiunga mkono kwa vitendo.

"Kwa hapa Wilaya ya Mwanga naomba nikutoe wasiwasi, sisi tuko vizuri, tuna mipango mizuri, tunashirikiana na viongozi kuanzia ngazi ya wilaya hadi mkoa, na tuna bahati moja , wananchi wetu wanaipenda CCM," alisema Dk. Maghembe.

Akieleza kuhusu mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Dk. Maghembe alitaja utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ukiwemo mradi wa Same–Mwanga–Korogwe uliokuwa umesimama kwa muda mrefu.

"Rais Samia aliukuta mradi ule ukiwa umesimama, lkini kwa mapenzi yake makubwa kwetu, alitafuta shilingi bilioni 161 na kuukamilisha, Mama aliweka pembeni shughuli zake na kuja Mwanga kutuzindulia mradi huu," alieleza.

Aidha, Dk. Maghembe alisema kuwa katika kipindi hicho, serikali ilitoa zaidi ya shilingi bilioni 4.4 ambazo zimesaidia kujenga hospitali mpya ya wilaya ikiwa na majengo 10 ambayo tayari yameanza kutoa huduma kwa wananchi.

Vilevile, alibainisha kuwa serikali ilitoa shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA), pamoja na shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala.

"Serikali pia ilitoa shilingi milioni 700 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya CD-Msuya, pamoja na shilingi bilioni 60 zilizotolewa kwa maendeleo katika Halmashauri ya Mwanga," alisema.

Dk. Maghembe alihitimisha kwa kusema kuwa mafanikio hayo yote ni ushahidi wa namna CCM ilivyojipanga kuwaletea maendeleo wananchi wa Mwanga na Tanzania kwa ujumla.










Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.