ALHAJI ALLY PENDO, AIBUKA KIDEDEA KURA ZA MAONI KATA YA MSARANGA

Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Katibu wa Elimu, Malezi na Mazingira kupitia Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Moshi Mjini, Alhaji Ally Pendo (maarufu kama Dunga), ameibuka mshindi katika kura za maoni za kuwania nafasi ya udiwani kupitia CCM katika Kata ya Msaranga, Manispaa ya Moshi.

Kura hizo za maoni zilifanyika Agosti 4, 2025 chini ya usimamizi wa chama, ambapo wagombea watatu walishiriki katika mchakato huo wa ndani ya CCM.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na wasimamizi wa uchaguzi wa chama hicho, Alhaji Ally Pendo alipata ushindi wa kishindo kwa kupata kura 120, akifuatiwa na Emanuel Mlingu aliyepata kura 20, huku Diwani aliyemaliza muda wake, Dkt. Charles Lyimo, akiambulia kura sifuri.

“Ushindi huu ni ishara ya imani kubwa waliyonayo wanachama kwangu na dira ya maendeleo niliyonayo kwa Kata ya Msaranga,” alisema Alhaji Pendo mara baada ya kutangazwa mshindi.

Kwa ushindi huo, Alhaji Pendo anaongoza katika mchakato wa kuwania nafasi ya kugombea udiwani kupitia tiketi ya CCM kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.

Mchakato wa kura za maoni ni sehemu ya mfumo wa ndani wa CCM unaolenga kuwapa wanachama nafasi ya kuchagua wagombea wanaowakilisha chama katika nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwa ni pamoja na urais, ubunge na udiwani.

Ushindi wa Alhaji Pendo umetafsiriwa na wachambuzi wa siasa za ndani ya chama hicho kuwa ni ishara ya kiu ya mabadiliko katika uongozi wa kata hiyo, hasa baada ya aliyekuwa diwani, Dkt. Lyimo, kushindwa kupata hata kura moja.

Wanachama wa CCM kata ya Msaranga sasa wanasubiri kwa hamu uamuzi wa ngazi za juu wa chama ili kuthibitisha jina la mgombea atakayepeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi huo.





Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.