MOSHI-KILIMANJARO.
Kampuni maarufu ya utalii nchini, Zara Tanzania Adventures, imezindua rasmi msimu wa tano wa kampeni yake ya kipekee ya “Twenzetu Kileleni 2025”, inayolenga kupanda Mlima Kilimanjaro kwa ajili ya kusherehekea miaka 64 ya Uhuru wa Tanganyika.
Uzinduzi huo umefanyika katika ofisi za kampuni hiyo mjini Moshi na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wadau wa utalii.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, alisifu mafanikio makubwa ya kampeni hiyo katika kuvutia watalii wa ndani na nje ya nchi.
“Kampeni hii imekuwa maarufu sana, tunapata wageni wengi, lakini hatuna mahali pa kuwaweka, wito wangu kwa Mkurugenzi Zainabu: kama fedha zipo, jenga hoteli nyingine, Watalii wanapata tabu kutoka Arusha kuja Kilimanjaro,” alisema Mkuu huyo wa mkoa.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Zara Tanzania Adventures, Zainabu Ansell, msimu huu wa kampeni unatarajiwa kuwahusisha zaidi ya watalii 200, wote wakishiriki kupanda Mlima Kilimanjaro kama sehemu ya kuenzi historia na uzalendo wa Taifa.
Naye Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA), Anjela Nyaki, alipongeza mchango endelevu wa kampuni hiyo katika kukuza sekta ya utalii na kuongeza mapato ya Taifa kupitia ongezeko la watalii.
Zoezi la kupanda mlima litafanyika kuanzia Desemba 5 hadi Desemba 10, 2025, ambapo litakuwa pia sehemu ya kuendeleza jitihada za kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania, hususan Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro, mlima ambao ni mrefu zaidi barani Afrika.
Kampeni ya “Twenzetu Kileleni”, ambayo sasa inaingia mwaka wake wa tano, imejikita katika kuhamasisha Watanzania na wageni kutoka mataifa mbalimbali kushiriki katika shughuli ya kupanda mlima kwa lengo la kusherehekea kumbukumbu ya uhuru na kutangaza utalii wa ndani.