SIHA-KILIMANJARO.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ali Ussi, amewasihi wananchi wa Wilaya ya Siha kuutunza, kuulinda na kuuenzi mradi wa maji wa skimu ya Lawate-Fuka-Gararagua-Kideko ili kuhakikisha unaleta manufaa ya kudumu kwa jamii.
Akizungumza jana wakati wa uzinduzi rasmi wa mradi huo katika eneo la Gararagua-Kideko, Ussi alisema mradi huo ni hazina kwa wananchi na unapaswa kulindwa kwa bidii na mshikamano wa kijamii.
“Mradi huu ni matokeo ya dhamira ya dhati ya serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya maji, hivyo ni jukumu letu sote kuulinda, kuutunza na kuhakikisha unadumu kwa vizazi vijavyo,” alisema Ussi.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Siha Mhandisi Mhandisi Elikalia Malisa, alisema mradi huo ulianza kutekelezwa mwezi Machi 2023 na kukamilika Septemba 2024 kwa gharama ya shilingi bilioni 2.3, ukifadhiliwa kupitia Mfuko wa Maji wa Taifa (National Water Fund) na fedha za Malipo kwa Matokeo (P4R).
Mhandisi Malisa, alisema kuwa mradi huo umeanza kutoa huduma kwa wakazi 7,828 wa vijiji sita vinavyonufaika moja kwa moja.
“Lengo kuu la mradi huu ni kuongeza na kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa maeneo haya, huku akisema kuwa mradi huo, umehusisha ujenzi wa banio la maji, tanki la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita 100,000, na pia umetoa ajira kwa watu 158 wakati wa utekelezaji wake,” alieleza Mhandisi Malisa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wa eneo hilo ulipo mradi huo Mwanaid Abuu na Grace Munuo, waliishukuru serikali kwa kukamilisha mradi huo, wakisema umeleta afueni kubwa kwa shughuli za maendeleo na maisha ya kila siku.
“Kupatikana kwa maji kumerahisisha sana maisha yetu, hatuhangaiki tena kutafuta maji mbali, sasa tuna muda zaidi wa kufanya kazi za maendeleo,” alisema Grace Munuo kwa furaha.
Mradi huo uliwekewa jiwe la msingi na mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2024, ikiwa ni ishara ya utekelezaji madhubuti wa miradi ya kimkakati inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
MWISHO.