MOSHI-KILIMANJARO.
Serikali imeipongeza kampuni ya utalii ya Zara Tanzania Adventures kwa kushinda tuzo ya kimataifa na kutambuliwa kama kampuni bora ya utalii inayoongoza Afrika, hatua iliyotajwa kuwa fahari kwa Tanzania na kichocheo kikubwa kwa maendeleo ya sekta ya utalii nchini.
Pongezi hizo zilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, wakati wa uzinduzi wa msimu wa tano wa kampeni ya Twende Zetu Kileleni, hafla iliyofanyika mjini Moshi mkoani humo.
“Tunajivunia mafanikio haya makubwa yaliyopatikana na Zara Tanzania Adventures, ushindi huu si wa kampuni pekee, bali ni wa Tanzania nzima, ni ushahidi kuwa tunayo uwezo mkubwa wa kuongoza katika sekta ya utalii kimataifa,” alisema RC Babu.
Amesema serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuunga mkono jitihada binafsi zinazolenga kuinua utalii, huku akisisitiza kuwa ushiriki wa Rais kwenye filamu ya The Royal Tour umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la watalii nchini.
Babu alieleza kuwa kampeni ya Twende Zetu Kileleni, iliyoanzishwa na Zara Tanzania Adventures kwa kushirikiana na TANAPA, imekuwa chombo muhimu katika kukuza utalii wa ndani, kuhifadhi mazingira, na kutoa ajira kwa Watanzania.
Aidha, alihImiza Watanzania kushiriki kikamilifu katika kupanda Mlima Kilimanjaro, akisema ni kivutio kilichopo nyumbani ambacho hakipaswi kuachwa kwa wageni pekee.
“Ni lazima tujifunze kuupenda mlima wetu, Watanzania wanapaswa kuwa mstari wa mbele kupanda Mlima Kilimanjaro kwani huu ni urithi wetu,” alisema.
Katika hotuba yake, Mkuu huyo wa mkoa, alitoa wito kwa Wawekezaji kuwekeza zaidi mkoani Kilimanjaro, hasa kwenye sekta ya huduma na utalii, huku akimtaka pia Mkurugenzi wa Zara kuendelea kuwekeza kwa kujenga hoteli kubwa ya kisasa itakayoboreshwa huduma za kitalii kwa wageni na wazawa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Zara Tanzania Adventures, Zainabu Ansell, alisema msimu huu wa tano wa kampeni ya Twende Zetu Kileleni umeboreshwa kwa kuongezwa huduma za afya kupitia clinics kwa wapandaji, na unatarajiwa kuvutia zaidi ya wageni 300 kutoka mataifa mbalimbali, pamoja na ushiriki wa Watanzania wengi zaidi.
Naye Meneja Rasilimali Watu wa kampuni hiyo Bernard Saini, alisema kampeni ya mwaka huu itafanyika Desemba 5 hadi 10, 2025, huku uzinduzi wa mapema ukilenga kutoa nafasi kwa mabadiliko ya ratiba kutokana na uchaguzi mkuu ujao.
Naye Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA), Anjela Nyaki, alipongeza mchango wa Zara Tanzania Adventure katika kukuza utalii na kuongeza mapato ya Taifa kupitia idadi kubwa ya watalii wanaowaleta kila mwaka.