MTIKISIKO WA KISIASA: VIJANA WATINGA KWA WINGI KUGOMBEA NDANI YA CCM

MOSHI-KILIMANJARO.

Katika kile kinachoonekana kuwa ni mwelekeo mpya wa kisiasa nchini, idadi kubwa ya vijana imejitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi za ubunge na udiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakilenga kupewa ridhaa ya kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao.

Mwitikio huu unaonesha ari ya vijana kushiriki moja kwa moja katika kuchochea mabadiliko ya kisera na maendeleo ya jamii zao kupitia uongozi wa kisiasa.

Kwa miaka mingi, vijana wamekuwa wakihimizwa kuingia kwenye siasa, lakini mara nyingi walikumbwa na changamoto kama vile mfumo kandamizi, ukosefu wa uzoefu, au kutokuaminiwa na vyama vya siasa. Hata hivyo, hali imebadilika: vijana na wanawake wanaonekana kupewa nafasi zaidi, na vyama navyo vinaonyesha mtazamo mpya.

Wachambuzi wa siasa wanasema mabadiliko haya ni kiashiria cha jinsi vijana wanavyotambua kuwa siasa ni nyenzo halali ya kuleta maendeleo, tofauti na mtazamo wa awali kuwa siasa ni kazi ya wazee pekee. Sasa vijana wanajiamini, wakiamini kuwa wao pia wana uwezo wa kuleta mageuzi ya kweli.

Katika mikoa kama Kilimanjaro, Morogoro, Dodoma, Mwanza na Mbeya, misururu ya vijana imejitokeza kwenye vituo vya kuchukulia fomu, wengine wakiwa wanashiriki kwa mara ya kwanza kabisa katika maisha yao ya kisiasa.

Baadhi ya vijana hao tayari walikuwa wakijihusisha na miradi ya kijamii na maendeleo, na sasa wanaona siasa kama jukwaa rasmi la kupanua mchango wao katika jamii.

Mmoja wa vijana waliowasilisha fomu za kugombea nafasi ya udiwani katika Kata ya Mwanga Mjini ni Ezekiel Dembere, mwenye Shahada mbili za Umahiri, moja kutoka China katika Uongozi wa Umma, na nyingine ya Sayansi ya Mazingira kutoka UDSM, pamoja na Shahada ya Elimu ya Jiografia na Kiingereza.

"Nilitangaza nia ya kugombea kwa sababu naamini vijana wakiendelea kusubiri, watabaki kuwa watazamaji. Tuna wajibu wa kuleta mabadiliko kwa vitendo," alisema Dembere.

Anaongeza kuwa vijana ni nguzo muhimu ya jamii yoyote. Akirejea mafundisho ya dini ya Kiislamu, anasema Qur’ani na hadithi za Mtume Muhammad (SAW) zinatambua nafasi muhimu ya vijana katika mageuzi ya kijamii.

Amin Ally Twaha, Kada wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini, amerejea tena katika mbio za kuwania ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini, baada ya kushiriki mchakato wa mwaka 2020 na kushika nafasi ya sita kati ya wagombea 36.

“Nina uzoefu, maono, na dhamira ya dhati kulitumikia jimbo hili, mwaka huu nina imani nitapata ridhaa ya chama,” alisema Twaha.

Anarejea historia ya harakati za kisiasa akiwataja waasisi wa taifa kama Mwalimu Julius Nyerere na Rashid Kawawa, waliokuwa vijana walipoanza safari ya kupigania uhuru hii, anasema, ni ishara kwamba msingi wa maendeleo na uhuru wa taifa huu ulijengwa na vijana.

Azack Ngowi, Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi CCM, amejitokeza pia kuwania ubunge wa Moshi Mjini, akisema ana dhamira ya kuwatumikia wananchi kwa moyo wa uzalendo.

Mchumi na msomi kutoka UDSM, Amiri Mkufya, ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya Young CEO Round Table Africa, amerejea kugombea Ubunge wa Jimbo la Mlalo kupitia CCM. anasema:

“Jimbo la Mlalo linahitaji fikra mbadala na uongozi wa maendeleo ya kweli. Niko tayari kulitumikia kwa maarifa na uzoefu wangu.”

WASOMI NA WANAWAKE VIONGOZI WAJITOKEZA KWA WINGI

Kwa upande mwingine, Prof. Neema Kumburu, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), naye amechukua fomu ya kuwania ubunge Moshi Mjini. Anasema:

“Umefika wakati wanawake wasomi tulichukue nafasi hizi za uongozi kwa weledi na dira ya maendeleo.”

Wanawake wengine kama Teresia Komba, wanasisitiza kuwa ni muda wa sauti ya mwanamke kusikika katika ngazi za maamuzi, wanawake wasomi wamejitokeza kwa wingi, wakihamasisha ushiriki jumuishi.

CCM YAJIPANGA KWA MCHAKATO WA HAKI NA UWAZI;

Frida Kaaya, Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini, amesema chama hicho kimeweka utaratibu wa haki na uwazi kuhakikisha kila mwanachama mwenye sifa anapata fursa ya kushiriki mchakato huu bila upendeleo.

“Tunazingatia misingi ya kidemokrasia ya ndani ya chama, ili kuhakikisha kila mmoja anashiriki kwa usawa,” alisema.

Pamoja na changamoto kama ukosefu wa rasilimali za kampeni na miundombinu ya kisiasa, vijana wanaonekana kuwa tayari kuvuka vizingiti hivyo ili kutoa mchango wao kwa taifa.

Mwitikio huu wa vijana kugombea nafasi za uongozi si jambo la kawaida ni dalili ya mabadiliko makubwa ya kisiasa nchini, kupitia mawazo mapya na nguvu ya kutenda, vijana hawa wana nafasi ya kuwa chachu ya maendeleo ya kweli.

Ni jukumu la vyama vya siasa, serikali, na jamii kwa ujumla kuhakikisha kuwa mazingira ya kisiasa yanabaki kuwa wazi, jumuishi, na yenye kuhimiza ushiriki wa vijana, kwani wao ndio nguzo ya leo na kesho ya Tanzania.






Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.