MLALO-LUSHOTO.
Mshindi wa Tuzo ya Young CEO Round Table Africa, mchumi na msomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Amiri Mkufya, anayefahamika pia kwa jina maarufu (Amesco), amejiunga rasmi kwa mara nyingine katika mbio za kuwania Ubunge wa Jimbo la Mlalo, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya kuchukua na kurejesha fomu ya kugombea nafasi hiyo.
Mkufya, ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, anatarajiwa kuleta ushindani mkali dhidi ya Mbunge wa sasa wa jimbo hilo, Rashid Shangazi, katika mchakato wa kura za maoni ndani ya chama hicho.
Hatua yake ya kurejea kwenye kinyang’anyiro hicho imeibua mjadala mpana miongoni mwa wanachama wa CCM na wananchi wa Mlalo, wakitaja wasifu wake wa kitaaluma na mafanikio nje ya siasa kama sababu inayompa mvuto wa kipekee.
“Jimbo la Mlalo linahitaji nguvu mpya, fikra mbadala na uongozi wenye dira ya maendeleo ya kweli, nimeamua kutumia maarifa na uzoefu wangu kuchangia ustawi wa wananchi wa Mlalo,” alisema Mkufya mara baada ya kurejesha fomu yake.
Tuzo ya Young CEO Round Table Africa aliyoshinda inamhusisha na safu ya viongozi chipukizi barani Afrika wanaotambuliwa kwa mchango wao katika uongozi, ubunifu wa kiuchumi na mabadiliko ya kijamii, jambo linalompa heshima ya kipekee katika ulingo wa siasa za maendeleo.
Dirisha la uchukuaji na urejeshaji wa fomu ndani ya CCM kwa nafasi za Ubunge na Udiwani lilifungwa rasmi Julai 2, 2025, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.