MOSHI-KILIMANJARO.
Takribani watu 3,000 wanatarajiwa kushiriki katika Tamasha la Filamu la Kilimanjaro (Kilimanjaro Film Festival 2025), linaloendelea kufanyika mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, likiwa ni sehemu ya harakati za kuikuza sekta ya filamu barani Afrika, huku pia likibeba kwa dhati ajenda ya utalii na utamaduni wa Tanzania.
Mkurugenzi wa tamasha hilo, Naamala Samson, akizungumza na waandishi wa habari Julai 4, 2025, alisema (KFF-2025) limekuwa jukwaa mahsusi kwa wadau wa filamu kutoka ndani na nje ya Afrika kubadilishana maarifa, kuimarisha ushirikiano wa kitaalamu, na kutoa sauti mpya kwa simulizi za bara hili.
“Tunapitia hadithi zetu kwa macho ya Kiafrika na kuyatangaza mandhari yetu kwa njia ya kipekee kupitia filamu, tumasha hili si tu tukio la sanaa, bali pia ni daraja la kutangaza vivutio vyetu vya utalii na kuhamasisha fahari ya kiutamaduni,” alisema Naamala.
Kwa mujibu wa Samson, tamasha hilo limeunganishwa moja kwa moja na ajenda ya kitaifa ya kutangaza utalii kupitia ubunifu wa kisanaa.
Alieleza kuwa Julai 5, 2025 kutafanyika ziara maalum ya washiriki, wakiwemo waandishi wa filamu, waigizaji na waongozaji, katika msitu wa Rau kwa ushirikiano na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Wilaya ya Moshi.
Alisema ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za kutangaza utalii wa kiikolojia kwa njia ya vitendo, ikilenga kuwapa wasanii msukumo wa kutumia mazingira halisi ya Tanzania katika kazi zao za ubunifu.
Aidha, tamasha hilo limejikita katika kuonesha filamu na picha zinazobeba mandhari ya kiutalii, ambapo zaidi ya picha 28 za vivutio vya asili na urithi wa Tanzania zitachorwa na kuoneshwa katika maonyesho rasmi ya tamasha hilo.
Matukio mengine makuu yanayofanyika katika viwanja vya John Shule Park, Karanga Magereza, ni pamoja na mafunzo kwa vijana kuhusu uandishi wa hadithi, uongozaji, na matumizi ya teknolojia ya kisasa ya filamu. Vilevile, Soko la Maudhui limeandaliwa kuwa jukwaa la majadiliano kati ya watayarishaji wa filamu, wawekezaji, wanunuzi na wasambazaji wa kazi za sanaa.
Pia kutakuwa na maonyesho ya mitindo, kazi za mikono, vyakula vya asili, sanaa ya picha, shughuli za uhifadhi wa mazingira, na utambulisho wa utamaduni wa Zanzibar pamoja na Tanzania Bara, huku Tamasha hilo la Kilimanjaro Film Festival linatarajiwa kufikia tamati Julai 6, 2025.