WANANCHI 3,000 WAONDOKANA NA ADHA YA MAJI

LANG'ATA-MWANGA.

Zaidi ya wananchi 3,000 wa Kijiji cha Lang’ata-Bora, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, wameondokana na tatizo sugu la upatikanaji wa maji baada ya serikali kupitia Wizara ya Maji kutoa Sh milioni 80 kwa ajili ya kuchimba kisima kirefu cha maji katika kijiji hicho.

Mradi huo muhimu ulizinduliwa rasmi Julai 1, 2025 na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ali Ussi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kutekeleza dira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya “kumtua mama ndoo kichwani”.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Ussi alitoa wito kwa wananchi kuulinda na kuutunza mradi huo ili uwe endelevu na kuendelea kutoa huduma muhimu ya maji kwa jamii.

"Serikali imewekeza fedha nyingi kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata maji safi na salama, ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha miundombinu hii inalindwa," alisema Ussi.

Alisema mradi huo ni sehemu ya mpango mkubwa wa kitaifa wa kuchimba visima 900 unaolenga kuhakikisha zaidi ya asilimia 85 ya wananchi waishio  vijijini wanapata huduma ya maji, hasa katika maeneo yenye changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma hiyo.

Kiongozi huyo pia alimtaja Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Wakili Joseph Tadayo, kuwa miongoni mwa viongozi waliopigania kwa juhudi mradi huo kutekelezwa.

"Mbunge huyu alikuwa mstari wa mbele bungeni kutetea miradi ya maendeleo, hususan ya maji. Mwenge wa Uhuru unampongeza kwa juhudi zake na pia baraza la madiwani kwa ushirikiano wao," aliongeza.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Weransari Munis, alisema mradi huo umetokana na uwekezaji mkubwa wa serikali ambao ulijumuisha ununuzi wa mtambo wa kuchimba visima wenye thamani ya Sh milioni 600.

"Mbali na kuchimba visima, RUWASA pia inasambaza maji hadi kwenye makazi ya wananchi, hii ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais kuhakikisha maeneo yenye changamoto ya maji yanapatiwa huduma hiyo muhimu," alisema Mhandisi Munis.

Wakazi wa kijiji hicho wameelezea furaha yao baada ya kuanza kunufaika na huduma hiyo, wakisema kwa miaka mingi wamekuwa wakitumia maji yasiyo salama hasa kipindi cha kiangazi na mvua, hali iliyosababisha magonjwa ya tumbo na milipuko ya magonjwa.

"Tulilazimika kutumia maji ya Bwawa la Nyumba ya Mungu ambayo hayakuwa salama, tuliugua sana," alisema Theresia John, mkazi wa kijiji hicho.

"Tunamshukuru Rais Samia, Mbunge wetu Tadayo na Diwani wetu kwa kuhakikisha tunapata maji safi, kisima hiki kimetufungua kutoka kwenye adha ya miaka mingi," alisema Haji Nassor Mwanga.

"Miaka ya nyuma kipindi cha mvua kulikuwa na mlipuko wa magonjwa, lakini mwaka huu tumepita salama kwa sababu ya mradi huu," alisema Beatrice John.

Mradi wa Lang’ata-Bora unaakisi dhamira ya serikali kuboresha maisha ya wananchi wa vijijini kupitia upatikanaji wa huduma za msingi kama maji, na ni ushahidi wa athari chanya za uwekezaji wa miradi ya maendeleo katika ngazi ya jamii.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.