KILIMO CHA KAHAWA CHAANZA KUZAA MATUNDA

DODOMA.

Katika juhudi za kukuza sekta ya Kahawa nchini, serikali imeongeza bajeti ya kilimo hadi kufikia Shilingi trilioni 1.3 kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwa ni hatua ya kuboresha upatikanaji wa pembejeo, huduma za ugani, na kuongeza tija kwa wakulima.

Taarifa hiyo imetolewa na Waziri George Simbachawene katika Mkutano Mkuu wa 15 wa Wadau wa Kahawa jijini Dodoma, ambapo alisisitiza dhamira ya serikali kufufua na kuendeleza mazao ya kimkakati ikiwemo kahawa.

"Serikali imeongeza bajeti ya sekta ya kilimo kutoka Shilingi bilioni 294 mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia Shilingi trilioni 1.3 kwa mwaka wa fedha 2025/2026, hii  ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuinua uzalishaji wa mazao ya kimkakati likiwemo zao la kahawa,"alisema SImbachawene.

Alisema serikali imeweka mkazo huo ili  kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo bora kwa wakati, ikiwemo mbegu, mbolea, huduma za ugani na miundombinu ya umwagiliaji, ili kuongeza tija na ubora wa kahawa inayozalishwa nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Primus Kimaryo, alisema licha ya lengo la taifa kuzalisha tani 300,000 za kahawa kwa mwaka, hadi sasa uzalishaji umefikia tani 85,000 pekee.

"Tunaendelea kufanya mapitio ya kina na tumeamua kuchukua hatua madhubuti, ikiwa ni pamoja na kugawa miche milioni 20 bure kwa wakulima, kupanua mashamba, na kufufua miti ya kahawa iliyozeeka ili ichipue upya," alisema Kimaryo.

Aidha, alibainisha kuwa TCB kwa kushirikiana na halmashauri mbalimbali, inaendesha mafunzo kwa maafisa ugani ili kuhakikisha wanawafikia wakulima kwa ufanisi zaidi.

Mmoja wa wakulima walioshiriki mkutano huo, Respicious John, alieleza kuwa ni wakati muafaka kwa vijana kuwekeza kwenye kilimo cha kahawa, akisisitiza kuwa sekta hiyo ina fursa nyingi za kiuchumi.

“Mwaka uliopita pekee, mkoa wa Kagera uliingiza Shilingi milioni 250 kupitia mauzo ya kahawa, huku akitoa wito kwa vijana kujitokeza, tutafikia malengo ya uzalishaji na kuinua maisha ya wengi,” alisema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.