TANZANIA YASHIKA NAFASI YA TATU YA UZALISHAJI WA KAHAWA

DODOMA.

Tanzania imepanda hadi nafasi ya tatu barani Afrika kwa uzalishaji wa kahawa, hatua iliyoiwezesha kuzipiku nchi za Kenya na Ivory Coast ambazo awali zilikuwa miongoni mwa vinara wa zao hilo barani humo.

Taarifa hiyo imetolewa Julai 5, 2025 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Ushirika na Umwagiliaji, Dkt. Stephen Nindi, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 15 wa Bodi ya Kahawa (TCB) uliofanyika jijini Dodoma.

Dkt. Nindi alisema kuwa serikali itaendelea kutafuta masoko ya uhakika ya kahawa katika mataifa mbalimbali ndani na nje ya Afrika ili kuhakikisha wakulima wa Tanzania wanaongeza kipato na taifa linapata mapato ya uhakika kupitia mauzo ya kahawa.

“Lengo letu ni kuhakikisha kahawa ya Tanzania inazidi kupata nafasi katika masoko ya kimataifa, na kuonekana katika kila kona ya dunia,” alisema Dkt. Nindi.

Aliagiza vyama vya ushirika kushirikiana kwa karibu na Bodi ya Kahawa ili kuondoa changamoto zinazowakabili wakulima, na kuhakikisha tasnia ya kahawa inakuwa imara, endelevu, na yenye tija kwa uchumi wa taifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Primus Kimaryo, alisema bodi hiyo inaendelea kutekeleza mikakati ya kukuza na kuimarisha uzalishaji wa kahawa ili kufikia malengo yaliyowekwa.

“Tuliweka malengo ya kuzalisha tani 300,000 ndani ya miaka mitano. Ingawa hatujafika huko bado, tumerudi kujipanga upya ili kuhakikisha tunayafikia,” alisema Kimaryo.

Aliongeza kuwa Bodi ya Kahawa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo maafisa ugani, wakulima, na halmashauri, kuhakikisha uzalishaji wa kahawa unachangia kikamilifu katika pato la taifa.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.