DAE ES SALAAM
Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) imeongeza uzalishaji wa miche ya kahawa kutoka miche 6,000 hadi kufikia miche 31,000, ikiwa ni hatua ya awali kuelekea lengo la kuzalisha miche milioni 40 itakayogawiwa bure kwa wakulima kote nchini.
Mkurugenzi wa Masoko wa TCB, Frank Nyarusi, alitoa taarifa hiyo jana alipokuwa akizungumza katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa mpango huo ni sehemu ya mkakati wa bodi hiyo wa kuongeza uzalishaji wa kahawa nchini, sambamba na kuwawezesha wakulima wadogo kuongeza tija katika shughuli zao za kilimo.
"Tunawaomba wakulima wachangamkie fursa hii kwa kuongeza mashamba yao. Kahawa inalipa, na mkulima anayejituma anaweza kubadili maisha yake kupitia zao hili, Kahawa ni moja ya mazao ya kimkakati yanayochangia kukuza pato la taifa," alisema Nyarusi.
Aidha, aliwataka Watanzania, hususan vijana, kuchangamkia fursa zilizopo katika mnyororo wa thamani wa zao hilo.
Licha ya Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa kahawa barani Afrika, Nyarusi alisema kiwango cha unywaji wa kahawa nchini bado kiko chini, hali ambayo imetokana na upotoshaji kuhusu faida za kahawa kiafya na kibiashara.
"Kuna kampuni nyingi zinazozalisha kahawa, lakini sisi tupo hapa kuwaelimisha Watanzania kuhusu utengenezaji wa kahawa bora na faida zake. Watu wengi hawanywi kahawa kwa sababu wamepotoshwa na taarifa zisizo sahihi," aliongeza.
Kwa mujibu wa Nyarusi, jukumu kuu la TCB katika maonesho hayo ni kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa zao la kahawa na kuhamasisha vijana kujiunga na shughuli za uzalishaji na biashara ya kahawa.
Alieleza kuwa bodi hiyo imeanzisha mpango maalum unaoitwa Kahawa Mkononi, unaolenga kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia biashara ya kahawa mijini.
Kupitia mpango huo, pikipiki za mizigo (bajaji) maalum zimeandaliwa kwa kushirikiana na benki zinazotoa mikopo yenye riba nafuu. Bajaji hizo zimefungwa vifaa vyote vinavyohitajika kwa ajili ya uandaaji na uuzaji wa kahawa mitaani.
"Si lazima uende shambani ili kufaidika na zao la kahawa. Kupitia Kahawa Mkononi, kijana anaweza kuingia kwenye mnyororo wa thamani wa kahawa kupitia ujasiriamali wa mijini na hivyo kuchangia pato la taifa," alisema.
Nyarusi alisema mpango huo umekuwa na mafanikio makubwa, kwani umeongeza hamasa kwa vijana kujiunga na sekta ya kahawa, ambayo inaendelea kukua kwa kasi nchini.
"Kahawa inalipa. Ndiyo maana sasa tumepanda kutoka nafasi ya tano hadi nafasi ya tatu kwa uzalishaji wa kahawa Afrika, tukizipita nchi kama Kenya. Lengo letu ni kuwa wauzaji wakuu wa kahawa barani Afrika," alieleza.
Aidha, alibainisha kuwa Tanzania ina bahati ya kuwa na mikoa mingi yenye uwezo wa kuzalisha aina mbalimbali za kahawa, hali inayoiweka nchi katika nafasi nzuri ya kuongoza soko la kahawa barani Afrika na kimataifa.
"Wito wangu kwa wakulima kote nchini ni kuzingatia kanuni bora za kilimo cha kahawa ili kuongeza ubora wa mazao yao na kuweza kushindana katika soko la kimataifa," alisisitiza.



