WAJUMBE WA UWT WATAKIWA KUEPUKA MAKUNDI BAADA YA UCHAGUZI Ruwaichi Kaale: "Umoja wetu ndio ushindi wetu"


MOSHI-KILIMANJARO.

Wajumbe wa mkutano mkuu maalumu wa Uchaguzi wa Udiwani wa Viti Maalumu kutoka Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Wilaya ya Moshi Vijijini wametakiwa kutoendekeza makundi au migawanyiko baada ya uchaguzi kumalizika.

Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa UWT Wilaya hiyo, Ruwaichi Kaale, wakati akifungua rasmi mkutano huo wa uchaguzi uliofanyika Julai 20,205, Kaale alisema kuwa mchakato wa uchaguzi una mshindani mmoja atakayeshinda, lakini wote wanapaswa kubaki kama wamoja kwa maslahi ya chama.

"Ni muhimu tukatambua kuwa ushindani ni wa muda mfupi, lakini chama chetu na uhusiano wetu ni wa kudumu, hatuwezi kujenga chama kwa misingi ya makundi, chuki au visasi," alisisitiza  Kaale.

Alisema ni kawaida katika uchaguzi baadhi ya majina kutopitishwa, lakini walioathirika hawapaswi kukata tamaa bali waendelee kushiriki katika shughuli za chama kwa bidii na uaminifu.

"Tunataka kuwa na chama imara, na hilo linawezekana tu endapo kila mmoja atakubali matokeo na kuendelea kuwa sehemu ya harakati za kujenga jumuiya yetu," aliongeza.

Uchaguzi huo ni sehemu ya mchakato wa ndani ya CCM unaolenga kuwapa nafasi wanawake kushiriki uongozi kupitia viti maalumu, hatua inayolenga kuimarisha usawa wa kijinsia na ushiriki wa wanawake katika maamuzi ya kisiasa.

Akizungumzia uchaguzi huo Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini, Ramadhani Mahanyu, alisema kuwa kila mjumbe alipiga kura kwa wagombea watatu, na kuongeza kuwa hatua inayofuata ni vikao vya uchujaji kabla ya majina kupelekwa ngazi za juu kwa uamuzi wa mwisho.

Mahanyu ambaye alikuwa Msimamizi msaidizi wa uchaguzi huo, alisema licha ya kupata washindi katika kuchaguzi huo bado michakato inaendelea kwani baada ya hapo viko vya uchujaji, na mwisho wa siku uteuzi utategemea na ushindi wa chama kwenye nafasi za udiwani kwenye kila kata.

Naye Katibu wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Wilaya ya Moshi Vijijini, Oliver Ngalawa aliwapongeza wanawake wote walioshiriki mchakato huo, wakiwemo watu wenye ulemavu na vijana.

“Nimefarijika kuona rika zote wakijitokeza katika walioongoza kwa kura wapo watu wenye ulemavu wawili, kundi la vijana watatu na watu wenye umri mkubwa, naendelea kuhamasisha wanawake kuchangamkia fursa hizi bila hofu,” alisema Ngalawa.

Mchujo wa kura za maoni kwa nafasi ya Madiwani wa Viti Maalum ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Moshi Vijijini umekamilika huku madiwani saba waliokuwa wakitetea nafasi zao wakipoteza nafasi hiyo, huku wagombea wawili wenye ulemavu wakifanikiwa kung'ara na kuingia kwenye orodha ya wanaoongoza.

Uchaguzi huo uliofanyika Julai 20, 2025 katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, ulisimamiwa na Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) msimamizi wa uchaguzi huo Constansia John,  alisema jumla ya wagombea 32 walishiriki katika uchaguzi huo, wakitokea katika tarafa nne za Kibosho, Vunjo Magharibi, Vunjo Mashariki na Hai Mashariki.

John ambaye pia ni Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Kilimanjaro alisema, madiwani waliotetea nafasi zao na kufanikiwa kuongoza ni Jenipha Chuwa ambaye pia ni mtu mwenye ulemavu (1,150 kura), Irine Mariki (1,090), Gladness Mbwambo (1,037) na Jenipha Nyambo (732).

Sura mpya zilizoibuka na kushinda ni Ester Kway (1,283), Pamela Chuwa (1,073), Sheila Mongi (1,062), Asia Primus Kimaryo (846), Athanasia Asenga ambaye pia ni mtu mwenye ulemavu (808), Dorine Mkandara (738), Messe Mndeme (635), na Kantate Mushi (589).

Aidha alisema madiwani waliokuwa wakitetea nafasi zao walishindwa kufurukuta katika mchujo huo ni pamoja na Aurelia Mushi (600), Anna Amani Lyimo (517), Mwajabu Mchovu (498), Fabiola Massawe (285), Theresia Mlay (235), Christina Mchau (207) na Adelina Temba (78).




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.