MOSHI-KILIMANJARO.
Kata za Msaranga, Mwika Kusini,
Rau, Mwika Kaskazini na Njiapanda zimeibuka kuwa miongoni mwa maeneo
yanayoongoza kwa matukio ya wizi wa mita za maji katika eneo la Manispaa na
wilaya ya Moshi kwa ujumla, ambapo jumla
ya mita 543 zenye thamani ya Sh milioni 65.1 zimeibiwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Taarifa hiyo imetolewa na
Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usimamizi wa Mazingira mjini Moshi (MUWSA),
Mhandisi Innocent Lugodisha, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini
kwake jana.
Kwa mujibu wa Mhandisi
Lugodisha, alisema wimbi hilo la wizi limesababisha hasara kubwa kwa mamlaka
hiyo na limekuwa likikwamisha juhudi za kuboresha huduma na miundombinu ya maji
kwa wananchi.
“Mita hizi ni ghali sana, kwani kila mita moja inauzwa Sh
120,000 na kama fedha zinazotumika kununua mita mpya zingetumika kwenye miradi mingine ya maendeleo ya huduma
ya maji, wananchi wangekuwa wamepata huduma bora zaidi kwa sasa,”alisema
Mhandsi Lugodisha.
Aidha, alieleza kuwa kila
inapong’olewa mita, maji huendelea kumwagika hovyo na kusababisha upotevu
mkubwa, hasa ikizingatiwa kuwa tayari maji hayo hutibiwa kwa gharama kubwa
kabla ya kufikishwa kwa mtumiaji wa mwisho.
“Tunapopoteza mita moja, si tu kwamba
huduma ya maji inakatika kwa mwananchi, bali pia tunapoteza maji yaliyotibiwa
kwa dawa, pamoja na nguvu kazi ya watumishi waliolipwa kuhakikisha maji
yanawafikia wananchi,”aliongeza.
Mbali na mita, Mhandisi
Lugodisha alibainisha kuwa pia kumekuwepo na wimbi la wizi wa mifuniko ya
chemba, ambapo chemba 850 zimeibiwa kwa kipindi hicho na vifaa hivyo kuuzwa kama vyuma chakavu kwa baadhi ya
wafanyabiashara.
Alisema takribani Sh milioni 765,
mamlaka imepata hasara kwa kuibiwa mifuniko ya chemba hizo, jambo ambalo
limekuwa likirudisha nyuma jitihada za
kusambaza huduma hiyo ya maji.
“Tunaendelea kufuatilia kwa
karibu wafanyabiashara wa vyuma chakavu, na yeyote atakayebainika kununua vifaa
vya wizi, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,”alionya.
Aliongeza kuwa “Katika
kukabiliana na tatizo hilo, MUWSA imechukua hatua ya kuanza kujenga chemba
zenye ulinzi zaidi kwa mujibu wa Mhandisi Lugodisha, katika mwaka wa fedha
2024/2025 tayari chemba 350 zimejengwa
kwa ajili ya kulinda mita zaidi ya 2,000 na awamu ya pili itahusisha
ujenzi wa chemba 500 kwa ulinzi wa mita zaidi ya 5,000.
Aidha alitoa wito kwa wananchi
kuendelea kushirikiana na mamlaka kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kukomesha
wizi huo unaohatarisha ustawi wa huduma ya maji kwa jamii nzima.
Kwa upande wake Mkurugenzi
mtendaji wa (MUWSA), Mhandisi Kija Limbe, alisema mpaka sasa mamlaka hiyo
imepata hasara kubwa kutokana na wizi wa miundombinu hiyo.
“Wako baadhi ya wananchi wasio waaminifu wamekuwa wakihujumu miundombinu hiyo na kuwaonya kuacha mara moja kwani kwa sasa serikali imeweka mbinu mbalimbali za kuwabaini na kuwakamata, sambamba na hatua stahiki kuchukuliwa dhidi yao wanaofanya vitendo hivyo vya kuhujumu miumbombinu ya maji, ambayo serikali inatumia fedha nyingi kwa ajili ya kuinunua ili kuhakikisha mwananchi anapata huduma ya maji karibu na eneo analioishi,”alisema Mhandisi Limbe.