SERIKALI KUJENGA KITUO CHA HUDUMA ZA UTENGAMAO KWA WARAIBU WA DAWA ZA KULEVYA MJINI MOSHI


MOSHI-KILIMANJARO.

Serikali ina mpango wa kujenga kituo kikubwa cha huduma za utengamao kwa Waraibu wa dawa za kulevya katika wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Hayo yameelezwa na Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini Priscus Tarimo, wakati wa uzinduzi wa mashindano ya Kombe la Zuberi (Zuberi Cup) kwa mwaka wa 2025, yaliyofanyika katika uwanja wa Reli, Kata ya Njoro, Manispaa ya Moshi, mkoani humo.

Alisema tayari serikali imetenga jumla ya Sh milioni 347, kwa ajili ya kujenga kituo cha huduma za utengemao kwa waraibu ambacho kitajengwa katika viwanja vya hospitali ya Moshi-Arusha kwa ajili ya kuwatibu waraibu, ili kusogeza karibu huduma hiyo ambayo ilikuwa inawalazimu kwenda Jijini Arusha kuifuata.

“Mamlaka hii ni taasisi ya serikali iliyo chini ya ofisi ya Waziri Mkuu na ambayo inashughulika na kuratibu masuala yanayohusiana na tatizo la dawa za kulevya hapa nchini”, alisema Mbunge Tarimo.

Aliendelea kusema kuwa hatua hiyo ni moja ya jitihada za dhati zinazofanywa na Serikali katika kupambana na kuimarisha huduma za tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya nchini.

Mbunge huyo alitoa shukrani zake kwa Serikali kwa kuitikia wito na hatimaye kuridhia kituo hicho ambacho alisema kitakuwa mkombozi wa waathirika wengi ambacho kinajenga mjini Moshi.

Alizungumzia sababu ya changamoto hiyo kuonekana kuweko Moshi, alisema inatokana na mji wa Moshi kuwa eneo la mpaka na nchi nyingine jambo linalopelekea dawa hizo kuingizwa nchini kutoka nje kwa urahisi.

Aidha, Tarimo alitoa wito kwa mamlaka mbalimbali likiwemo jeshi la polisi kuendelea kutoa elimu kuhusiana na athari za dawa za kulevya ili kuokoa nguvu kazi ya Taifa.

Kwa upande wake Mstahiki Meya mstaafu wa Manispaa ya Moshi Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, alisema uwepo wa kituo hicho unashabihiana na Dira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, inayoelekeza kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulenya, ikiwemo uimarishaji wa utoaji wa elimu kinga, pamoja na upanuzi wa tiba  na huduma za utengamao kwa waraibu wa dawa za kulevya nchini.

“Ninaishukuru sana Serikali kwa kukubali kituo hiki kujengwa katika Manispaa yetu ya Moshi, wito wangu kwa wazazi kuwa karibu na watoto wao na kuwafuatilia nyendo zao  ili kuweza kuzuia tatizo hili la dawa za kulevya katika ngazi ya familia na kuendelea kuwa na kizazi chenye afya bora na kujiletea maendeleo yao na taifa kwa ujumla,”alisema Mhandisi Kidumo.

Naye Mkurugenzi taasisi isiyo kuwa ya kiserikali ya Recovery Youth With Vision (REYOVI), Eliaza Ngoda, alisema kundi kubwa linaloathirika na matumizi ya dawa za kulevya ni lile la vijana wenye umri kati ya miaka 15-35.

Alisema changamoto hiyo ni kubwa na kwamba inatokana na vijana wengi kuiga wasanii haswa wale wa nje ya nchi ambao wanatumia dawa hizi hatari.

"Wanapowaona wasanii wakivuta na wao kundi hilo wanatamani kufanya hivyo wakiamini ya kuwa wasanii hao umaarufu wao unatokana na matumizi ya dawa hizo”, alisema.

Akizungumzia ujio wa kituo hicho Ngoda alisema kujengwa kwa.kituo.hicho kitatoa huduma bure kabisa na kwamba kundi kubwa la vijana litanufaika na huduma ambazo zinapatikana Jijini Arusha na kwamba kutokana na changamoto ya ufinyu wa fedha vijana wengi hawana uwezo wa kuzifuata Arusha.

WANANCHI WAPONGEZA HATUA HIYO;

Baadhi ya wakazi wa Moshi wameipongeza serikali kujenga kituo kikubwa cha huduma za utengamao kwa waraibu wa dawa za kulevya mjini hapa.

Mkazi wa Kata ya Longuo ‘B’ Michael Gadi Uronu, alisema “Madhara ya dawa za kulevya kwa vijana ni makubwa sana, yamewafanya vijana wengi washindwe kujitambua, wengi hawana tena uwezo wa kufikiri sawasawa, hata wakiwa na wazazi wao, hawasikilizi chochote kila kitu kwao ni sawa tu.” Alisema Uroni.

Naye mkazi wa kata ya Shirimatunda Muksini Ali, alipongeza serikali kwa kuona umuhimu wa kuwa na kituo hicho moshi, huku akisisitiza umuhimu wa kuhusisha viongozi wa kiroho katika utoaji wa huduma.

“Kunapokuwepo na malezi ya kiroho kutawajenga vijana katika misingi ya kiimani, na hivyo kuwasaidia kuacha kabisa kutumia dawa hizo,” alisema.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.