DODOMA-TANZANIA.
Taasisi isiyo ya kiserikali ya Recovery Youth With Vision (REYOVI), imepokea tuzo ya heshima kutoka Ubalozi wa Marekani kupitia Best HIV/AIDS Practice Awards 2024, ikiwa ni kutambua mchango wake mkubwa katika kupambana na matumizi ya dawa za kulevya na maambukizi ya virusi vya UKIMWI miongoni mwa vijana.
Akizungumza jana jijini Dodoma na Waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa REYOVI, Eliaza Ngoda, alisema tuzo hiyo ni matokeo ya kazi kubwa waliyoifanya katika kusaidia waraibu na makundi yaliyo hatarini kurejea kwenye maisha ya kawaida.
“Tumeweza kuwasaidia zaidi ya waraibu 200 waliokuwa wakitumia dawa aina ya cocaine na heroine, huku tukiwarudisha kazini waraibu tisa waliokuwa wamepoteza ajira kutokana na uraibu,” alisema Ngoda.
Kwa mujibu wa Ngoda, REYOVI pia imefanikiwa kuwapeleka shule watoto saba waliokuwa wameacha masomo na kujihusisha na kuombaomba mitaani, huku zaidi ya vijana 300 wameunganishwa na huduma za afya ya VVU, wakiwemo waliokuwa wakijihusisha na biashara ya ngono.
Katika juhudi za kuwawezesha kiuchumi, taasisi hiyo imetoa mafunzo ya ujasiriamali kwa waraibu 300, ambapo kati yao 70 tayari wameanzisha biashara ndogo ndogo zinazowaingizia kipato.
Vilevile, REYOVI imewasaidia wanawake 23 waliokuwa wakijihusisha na biashara ya ngono kuanzisha shughuli mbadala kama vile saluni na biashara ndani ya soko la 77.
Ngoda aliongeza kuwa taasisi hiyo pia imeanzisha mradi wa Sh milioni 500 kwa ajili ya kufanya uchambuzi wa hali za watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi katika kata tatu za Jiji la Dodoma, ikiwemo Kata ya Viwandani.
Akikabidhi Tuzo hiyo kwa niaba ya Ubalozi wa Marekani na Mkurugenzi kutoka Tanzanian Health Summit Organization, Anord Kaliua, aliwapongeza REYOVI kwa moyo wa kujitolea na kuwaomba waendelee kuleta ubunifu katika kusaidia jamii.
Kwa upande wao, wadau mbalimbali wa afya na maendeleo ya jamii, akiwemo Mratibu wa Ukimwi Mkoa wa Dodoma Dayz Kanyama, na Mwenyekiti wa Key Vulnerable Population Forum Taifa (KVP), Marineus Mutogore, walipongeza jitihada za REYOVI na kuitaka jamii kuunga mkono kazi inayofanywa na taasisi hiyo.






