MOSHI-KILIMANJARO.
Mstahiki Meya mstaafu wa halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, ameweka bayana azma yake ya kuendeleza michezo kwa wanawake kwa kujenga uwanja maalum wa netiboli, ili kuwapa fursa wanasoka wa kike kushiriki kikamilifu katika michuano mbalimbali.
Akizungumza jana na waandishi wa habari, Mhandisi Kidumo alisema mipango hiyo ni sehemu ya jitihada zake za kuhakikisha michezo inakuwa jumuishi na yenye tija kwa jamii yote.
"Tunahitaji kuhakikisha kuwa michezo si ya wanaume tu,wachezaji wa kike nao wanapaswa kuwa na maeneo yao rasmi ya kufanyia mazoezi na kuandaa mashindano," alisema Kidumo.
Katika mahojiano hayo, aligusia pia hatua kubwa ya maendeleo iliyopatikana katika uwanja wa Railway-Njoro, ambao ameujenga kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 10, huku akisema kuwa uwanja huo sasa umeboreshwa kwa kiwango kikubwa, ikiwemo uwekaji wa nyasi, ukarabati wa miundombinu ya kukaa kwa watazamaji, na kuboresha usalama wa maeneo ya kuangalia michezo.
Kidumo alisema kuwa maboresho hayo yameipa sura mpya Zuberi Cup Tournament 2025, ambayo inatarajiwa kuibua vipaji vipya na kutoa burudani kwa wakazi wa Moshi.
"Mashindano haya yamekuwa kivutio kikubwa kwa vijana, na kupitia uwanja huu mpya, tutakuwa na mazingira bora zaidi ya kuendesha michezo kwa utulivu na hadhi," alisisitiza.
Aidha, Mhandisi Kidumo ambaye pia ni Diwani mstaafu wa Kata ya Njoro, alibainisha kuwa baada ya mafanikio ya uwanja wa Railway-Njoro, nguvu sasa zinaelekezwa kwenye ukarabati wa uwanja wa Nelson Mandela uliopo eneo la Pasua, lengo, alisema, ni kuhakikisha kila kata ndani ya Manispaa ya Moshi inakuwa na uwanja wa michezo unaokidhi mahitaji ya jamii.
"Uwekezaji huu ni sehemu ya dira yetu ya kuona michezo inachangia katika kujenga afya, nidhamu, ajira, na mshikamano miongoni mwa wakazi wetu," aliongeza.












