AMIN ALLY TWAHA; AJITOSA TENA UBUNGE JIMBO LA MOSHI MJINI KUPITIA CCM

MOSHI, KILIMANJARO.

Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amin Ally Twaha, amejiunga rasmi na mbio za kuwania Ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini kwa mwaka 2025, baada ya kuchukua na kurejesha fomu mapema leo Julai 2, 2025.

Twaha alifika katika ofisi za CCM Wilaya ya Moshi Mjini majira ya saa 3:15 asubuhi, ambapo alipokelewa na Katibu wa CCM Wilaya hiyo Frida Kaaya, kabla ya kurejesha fomu yake, akitangaza nia ya kuomba ridhaa ya chama ili kupeperusha bendera ya CCM kwenye uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Dirisha la uchukuaji fomu kwa ajili ya nafasi mbalimbali ndani ya CCM lilifunguliwa rasmi Juni 28, 2025, na linawahusu wanachama wanaotaka kuwania nafasi za Ubunge na Udiwani kote nchini.

Amin Twaha si mgeni katika kinyang'anyiro cha kisiasa; katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, alijitosa kuwania ubunge wa jimbo hilo na kushika nafasi ya sita kati ya wagombea 36 waliokuwa wamejitokeza kuwania uteuzi wa CCM.

“Nina imani kubwa kuwa mwaka huu nitapata ridhaa ya chama changu kuwakilisha CCM kwenye nafasi ya Ubunge wa Moshi Mjini. Nina uzoefu, maono na dhamira ya dhati ya kulitumikia jimbo hili,” alisema Twaha mara baada ya kurejesha fomu.

Wanachama wengine wa CCM wameendelea kujitokeza kurejesha fomu za kugombea nafasi mbalimbali, huku ushindani ukiwa mkubwa katika baadhi ya majimbo, ikiwemo Moshi Mjini ambayo ni ngome muhimu kisiasa katika mkoa wa Kilimanjaro.

Taarifa kutoka CCM zinasema kuwa mchakato wa kuchambua majina ya wagombea utaanza mara baada ya dirisha la uchukuaji na urejeshaji wa fomu kufungwa, ambapo jina moja litapitishwa kuwakilisha chama katika uchaguzi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.