MOSHI-KILIMANJARO.
Aliyekuwa mlinzi wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, na Diwani wa Kata ya Kiboriloni, Frank Kagoma, ametangaza rasmi kurejea Chama Cha Mapinduzi (CCM), akisema amechukua uamuzi huo ili kushirikiana na serikali kuwaletea wananchi maendeleo.
Akizungumza wakati wa hafla ya mapokezi iliyoandaliwa na uongozi wa CCM Wilaya ya Moshi, Kagoma alisema kuwa ameamua "kupanda gari la CCM" baada ya kuona safari ya maendeleo kupitia chama alichokuwepo imekwama.
“Gari nililokuwa nimelipanda limeharibikia Mto Ruvu, nikaona nipande gari la CCM ili liweze kunifikisha mapema kwenye safari ya kuwahudumia wananchi,” alisema Kagoma huku akibainisha kuwa baadhi ya waliokuwa wakisafiri naye pia walimshauri atafute njia nyingine.
Alieleza kuwa amejisikia faraja kujiunga na chama tawala kwa kuwa sasa ataweza kutekeleza majukumu yake ya udiwani kwa ufanisi zaidi kupitia jukwaa lenye ridhaa ya wananchi.
Kagoma pia alitumia fursa hiyo kumpongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Mwajuma Nasombe, kwa kumpa ushirikiano licha ya kuwa kutoka chama cha upinzani, alisema hali hiyo ilionyesha kuwa maendeleo hayapaswi kuwa na mipaka ya itikadi.
“Mkurugenzi na timu yake pamoja na Mstahiki Meya Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, walinipa ushirikiano mkubwa bila kujali chama nilichotoka, maendeleo katika kata yangu yalipatikana kama vile nilikuwa kutoka chama tawala,” aliongeza.
Kuhusu msukumo wa kurejea CCM, Kagoma alisifu juhudi za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akisema zimekuwa na matokeo chanya yanayoonekana wazi, hasa kwenye sekta ya miundombinu.
“Ninasafiri kutoka Dodoma saa tatu na nilifika Dar es Salaam saa 11 jioni jambo ambalo niliweza kutumia saa nane kufika Dar es Salaam, huu ni uthibitisho wa kazi nzuri inayofanywa na Rais Samia,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi, Faraj Swai, alimkaribisha Kagoma kwa moyo mkunjufu, akisema licha ya kuwa upinzani, alikuwa akishirikiana vizuri na viongozi wa CCM kutekeleza miradi ya maendeleo.
“Sijawahi kumsikia Kagoma akisema maneno yasiyo ya staha dhidi ya CCM, badala yake, alikuwa mstari wa mbele katika kutekeleza ilani ya maendeleo,” alisema Swai.
Naye Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo, alimpongeza kwa uamuzi wake wa kurejea CCM na kueleza kuwa Kagoma alikuwa nguzo muhimu ya maendeleo katika Kata ya Kiboriloni.
Alitaja baadhi ya miradi aliyoshiriki kama Diwani kuwa ni pamoja na ujenzi wa zahanati inayopandishwa hadhi kuwa kituo cha afya, ujenzi wa barabara za KDC-Mbokomu na KDC Sokoni hadi Shule ya Msingi Mbokomu kwa kiwango cha lami, pamoja na ujenzi wa madarasa kwa shule za msingi na sekondari.
“Nampongeza kwa uamuzi wake wa kujiunga na CCM. Tunaahidi kushirikiana naye ili kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo wanayotarajia,” alisema Bw. Tarimo.