TAMASHA LA KIMATAIFA LA FILAMU LA KILIMANJARO KUITANGAZA TANZANIA KIMATAIFA

MOSHI-KILIMANJARO.

Tamasha la Kimataifa la Filamu la Kilimanjaro (Kilimanjaro Film Festival) linatarajiwa kufanyika mjini Moshi kuanzia Julai 2 hadi 6, 2025, likiwa na lengo la kuibua mazao mapya ya utalii nchini na kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia filamu.

Zaidi ya kazi 3,000 za filamu kutoka nchi zaidi ya 135 zimewasilishwa kwa ajili ya kushiriki tamasha hilo, ambapo filamu 100 bora zimechaguliwa kuwania tuzo katika vipengele mbalimbali, tamasha hilo litafanyika kwenye viwanja vya John Shule Park, Karanga Magera, chini ya uenyekiti wa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, ambaye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Tamasha, Naamala Samson, tukio hilo linalenga kukuza vipaji vya wasanii wa ndani na wa kimataifa, kuimarisha utalii wa kitamaduni, pamoja na kujenga jukwaa la ubunifu na ushirikiano baina ya wadau wa filamu, utalii na teknolojia.

“Tamasha hili linakusudiwa kuwa la kila mwaka, linalenga si tu kutoa burudani bali pia kuwa kichocheo cha ukuaji wa sekta ya utalii wa filamu, ambao kwa sasa ni miongoni mwa sekta zinazokua kwa kasi duniani,” alisema Naamala.

Naamala aliongeza kuwa kupitia filamu, maeneo ya asili, historia, tamaduni na maisha halisi ya watu wa Tanzania yatatangazwa kimataifa, jambo litakaloongeza mvuto kwa watalii kuitembelea nchi hiyo.

Alisema tamasha hilo litajumuisha, maonyesho ya filamu za Kiafrika na kimataifa. midahalo ya kisanaa, warsha za mafunzo kwa vijana na wanahabari wa filamu, makongamano ya kitaalamu ya sekta ya utalii, sanaa na teknolojia.

“Tunaamini filamu ni daraja la mawasiliano la karne ya 21. Kupitia tamasha hili, tutawapa vijana fursa ya kujifunza, kuonyesha vipaji vyao, na kujijengea mitandao ya ushirikiano wa kimataifa,” aliongeza Naamala.

Tamasha linatarajiwa pia kuwa chanzo cha ajira kwa vijana, kuboresha mapato ya ndani kupitia wageni wa kimataifa, na kukuza matumizi ya lugha ya Kiswahili kimataifa kupitia filamu bora zinazoweza kushindanishwa kwenye majukwaa makubwa duniani.

Kwa mara nyingine, Tanzania inajidhihirisha kama kitovu cha ubunifu wa kitamaduni, ikiitumia filamu kama njia ya kusimulia hadithi zake kwa dunia nzima, hadithi ambazo sasa zitapitia macho ya kamera.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.