ABDALLAH THABIT AREJESHA FOMU YA UDIWANI SOWETO, AHAMASISHA VIJANA KUONGOZA KATA

MOSHI-MJINI

Mwenyekiti mstaafu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Wilaya ya Moshi Mjini, Abdallah Yushia Thabit, ameendelea kuonesha dhamira yake ya kisiasa baada ya kurejesha fomu ya kuomba ridhaa ya chama kuwania nafasi ya udiwani katika Kata ya Soweto, kupitia CCM.

Thabit alikabidhi fomu hiyo kwa Katibu wa CCM Kata ya Soweto, Alphonce Ikandilo, mnamo Julai 1, 2025, majira ya saa saba mchana katika ofisi za chama za kata hiyo.

Akizungumza mara baada ya kurejesha fomu, Thabit alisema kuwa sasa ni wakati wa vijana kupewa nafasi ya kuongoza na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii kwenye ngazi ya kata.

“Umefika wakati vijana tuchukue nafasi katika uongozi, tunayo nguvu, mawazo mapya na uwezo wa kushughulikia changamoto za wananchi kwa kasi na ubunifu,” alisema Thabit.

"Hii ni mara ya tatu kwa Thabit kuomba ridhaa ya chama kuwania udiwani katika kata hiyo, baada ya kufanya hivyo pia katika miaka ya 2015 na 2020, hatua inayoonesha uaminifu na uthabiti wake wa kisiasa ndani ya CCM na katika jamii ya Soweto".

Kwa mujibu wa ratiba ya chama, dirisha la uchukuaji na urejeshaji wa fomu linatarajiwa kufungwa Julai 2, 2025, ambapo hatua ya mchujo na majina ya mwisho ya wagombea watakaopeperusha bendera ya CCM yataainishwa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.