MOSHI-KILIMANJARO.
Aliyewahi kuwa Kamanda wa Hamasa na Chipukizi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Wilaya ya Moshi Mjini, Sajjad Ally Mshele, amejiunga rasmi na kinyang’anyiro cha kuwania ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya kurejesha fomu yake Julai 1, 2025.
Mshele alikabidhi fomu hiyo kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini, Frida Kaaya, katika ofisi za chama zilizopo mjini Moshi, akiomba ridhaa ya chama kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza baada ya kupokea fomu hiyo, Katibu wa CCM wilaya ya Moshi Mjini, Frida Kaaya, alisema ameridhishwa na nidhamu na mwitikio wa watia nia wanaojitokeza, hususan kwa kuzingatia maelekezo ya chama ya kutofuatana na makundi ya tarumbeta au shamrashamra zisizo rasmi wakati wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu.
“Tunawapongeza wote waliotii maagizo yaliyotolewa na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, kuhusu utaratibu wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu, mpaka sasa watia nia wameonesha ustaarabu wa hali ya juu,” alisema Frida Kaaya.
Dirisha la uchukuaji na urejeshaji wa fomu linatarajiwa kufungwa Julai 2, 2025, saa 10:00 jioni, ambapo mchakato wa mchujo wa awali utafuata, kabla ya chama kupendekeza jina la mgombea atakayepeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu.
Mshele anajiunga na orodha ya wagombea kadhaa waliojitokeza kuwania nafasi hiyo, ikiwa ni ishara ya ushindani mkali na uhamasishaji mkubwa ndani ya chama katika jimbo la Moshi Mjini.