UPEPO MPYA WA KISIASA: WANAWAKE WASOMI WAPIGANIA JIMBO LA MOSHI MJINI

MOSHI-MJINI.

Mchakato wa urejeshaji wa fomu za kuwania ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) umeendelea kushika kasi, huku wanawake wasomi wakijitokeza kwa wingi, wakionesha dhamira ya kulichukua jimbo la Moshi Mjini katika uchaguzi ujao.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), Kitivo cha Biashara na Sayansi za Mawasiliano, Prof. Neema Kumburu, ni miongoni mwa wanawake waliojitokeza leo Julai mosi,2025 na kurejesha fomu hiyo kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini, Frida Kaaya.

Prof. Kumburu alirejesha fomu hiyo majira ya saa nne asubuhi, akisisitiza kuwa umefika wakati wa wanawake wasomi kuchukua nafasi za uongozi na kulitumikia jimbo hilo kwa weledi na maono ya maendeleo.

“Umefika wakati wanawake wasomi tulichukue jimbo hili, tuna uwezo, tunayo elimu, na zaidi ya yote tuna dhamira ya kweli ya kulitumikia taifa kwa misingi ya haki, uwazi na maendeleo,” alisema Prof. Kumburu mara baada ya kurejesha fomu.

Kwa mujibu wa takwimu za awali kutoka ofisi ya CCM wilayani, idadi ya wanawake wanaojitokeza kuchukua na kurejesha fomu imeongezeka ikilinganishwa na miaka ya nyuma, jambo linaloashiria kuongezeka kwa hamasa ya kisiasa miongoni mwa wanawake, hasa wale wenye taaluma na elimu ya juu.

Wasomi wengine kutoka sekta mbalimbali nao wameanza kuonesha nia ya kuwania nafasi hiyo, hali inayoibua ushindani mkubwa ndani ya chama na kuongeza matarajio ya wananchi kupata uongozi bora na wenye dira.

Urejeshaji wa fomu unatarajiwa kukamilika Julai 2, 2025 majira ya saa kumi jioni, ambapo chama kitafanya mchujo wa awali kabla ya kupendekeza jina la mgombea atakayepeperusha bendera ya CCM kwenye uchaguzi mkuu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.