FRIDA MBERESERO ARUDISHA FOMU YA KUOMBA RIDHAA YA UBUNGE JIMBO LA MWANGA

MWANGA-KILIMANJARO.

Mwanasiasa na kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Frida Mberesero, amerudisha rasmi fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea ubunge katika Jimbo la Mwanga, mkoani Kilimanjaro, kwa uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025.

Akizungumza mara baada ya kurejesha fomu hiyo mbele ya waandishi wa habari, Mberesero amesema ameamua kuwania nafasi hiyo kwa lengo la kuleta maendeleo endelevu katika jimbo hilo, hususan kwenye maeneo ya elimu, afya na uwezeshaji wa vijana na wanawake.

“Nina dhamira ya dhati ya kulitumika Taifa kupitia Jimbo la Mwanga, naamini kwa ushirikiano na wananchi, tunaweza kuleta mabadiliko chanya katika sekta muhimu zinazogusa maisha ya kila siku ya watu wetu,” alisema.

Mberesero ameahidi kama chama kitamteua kugombea ubunge katika Jimbo hilo, ataendesha kampeni za kistaarabu na zinazojikita kwenye hoja na sera, huku akiwataka wananchi waendelee kudumisha amani na mshikamano wakati wote wa mchakato wa kisiasa.

Kwa sasa, Jimbo la Mwanga linaendelea kushuhudia ushindani mkali kutoka kwa wagombea mbalimbali wanaowania tiketi ya CCM kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.