MOSHI-KILIMANJARO.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ally Ussi, amempongeza Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Moshi (MUWSA), Mhandisi Kija Limbe, kwa uongozi thabiti na utekelezaji bora wa mradi mkubwa wa uzalishaji maji kupitia chanzo cha Karanga Darajani.
Mradi huo, ambao umegharimu Shilingi Bilioni 2.4 kutoka kwenye mapato ya ndani ya MUWSA, umezinduliwa rasmi na Mwenge wa Uhuru, ikiwa ni hatua kubwa ya kuhakikisha wakazi wa Moshi wanapata huduma ya maji safi na salama kwa uhakika.
Ussi alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo ni ushahidi tosha wa dhamira ya kweli ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, katika kuimarisha huduma za maji nchini.
“Ninampongeza sana Mkurugenzi wa MUWSA, Mhandisi Kija Limbe, kwa usimamizi na utekelezaji wa mradi huu mkubwa kwa kutumia wataalamu wa ndani na rasilimali za ndani, huu ni mfano wa kuigwa katika sekta ya maji na huduma kwa wananchi,” alisema Ussi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mhandisi Limbe, mradi huo umehusisha ujenzi wa chemba nne, chemba kuu ya kukusanyia maji kutoka chemichemi, mtaro wa kuzuia maji ya mvua, pamoja na ukuta wa kuzuia maji ya mto kuingia kwenye chanzo.
Aidha, bomba la nchi 10 limevushwa katika mto Karanga hadi tanki la Kilimanjaro umbali wa kilomita 2.3, sambamba na uwekaji wa pampu na fensi ya mitambo ya kusukuma maji.
"Mradi huo unatarajiwa kuhudumia wakazi takribani 230,784 kutoka kata za Kiboroloni, Msaranga, Mawenzi, Bondeni, Pasua, Bomambuzi, Majengo, na Mabogini".
Alisema Uzalishaji wa maji umeongezeka kwa zaidi ya mita za ujazo 3,888 kwa siku na masaa ya upatikanaji wa huduma hiyo yamefikia wastani wa saa 23.7 kwa siku.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo ni mafanikio ya kipekee yanayojivunia matumizi bora ya mapato ya ndani pamoja na uwezo wa wataalamu wa ndani wa MUWSA.
Mradi huu unaendelea kuleta matumaini makubwa kwa wananchi wa Moshi katika juhudi za kupata huduma endelevu ya maji safi na salama.