MOSHI-KILIMANJARO.
Wanachama mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameendelea kujitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi za uongozi kupitia uchaguzi mkuu ujao, wakiwania nafasi za ubunge na udiwani katika kata na majimbo tofauti ndani ya Wilaya ya Moshi Mjini.
Miongoni mwa waliojitokeza ni Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kiusa, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Khalid Shekoloa, ambaye amechukua fomu ya kugombea nafasi ya udiwani, akieleza kuwa amejipima kwa kina na kuona yuko tayari kuwatumikia wananchi.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu, Shekoloa alisema: “Nimeamua kufuata utaratibu wa chama, nimejipima kwa uhalisia wa kisiasa na kiu ya kuleta mageuzi chanya. Endapo nitapata ridhaa ya chama, nitaleta mabadiliko makubwa ya maendeleo katika Kata ya Kiusa.”
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini, Frida Kaaya, alieleza kuwa chama hicho kimejipanga vyema kuhakikisha mchakato wa uchukuaji fomu, kura za maoni na uteuzi wa wagombea unafanyika kwa haki, uwazi na kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
“CCM imeweka utaratibu wa haki unaozingatia misingi ya kidemokrasia ya ndani ya chama. tunahakikisha kila mwanachama mwenye sifa anapata fursa ya kushiriki mchakato huu bila upendeleo,” alisema Kaaya.
Zoezi la uchukuaji wa fomu ndani ya CCM limeibua hamasa kubwa kwa wanachama wanaotamani kushiriki uongozi wa kisiasa, jambo linalotajwa kuwa ishara ya uhai wa chama na ushiriki wa wananchi katika kujenga msingi wa maendeleo endelevu.