MOSHI-KILIMANJARO.
Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Moshi Mjini, Haji Fundi Haji, amejitokeza kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama chake ili kugombea nafasi ya udiwani katika Kata ya Bondeni kwenye Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka 2025.
Haji alichukua fomu hiyo mnamo Juni 30, 2025, majira ya saa nne asubuhi, katika ofisi za CCM Kata ya Bondeni, akieleza kuwa ana nia ya dhati ya kushirikiana na wananchi kuleta maendeleo ya kweli katika kata hiyo.
“Nimekuja kuchukua fomu ya kuwania udiwani Kata ya Bondeni, kiu yangu ni kuona nashirikiana na wenzangu katika kuleta maendeleo ya wananchi kwa ujumla,” alisema Haji mara baada ya kuchukua fomu.
"Hii ni mara ya pili kwa Haji kuwania nafasi hiyo, ambapo mwaka 2020 alishiriki katika mchakato wa kura za maoni ndani ya chama hicho na kushika nafasi ya tatu kati ya wagombea wanne waliotia nia".
Katika kura hizo za mwaka 2020, Haji alipata kura 12, huku Masiu Hamis Kilusu akiongoza kwa kura 15, akifuatiwa na Athuman Kala aliyepata kura 13, na Husein Msaki aliyeshika nafasi ya mwisho kwa kura 7.
Zoezi la uchukuaji wa fomu za kugombea nafasi za Udiwani na Ubunge ndani ya CCM linaendelea katika Wilaya ya Moshi Mjini, ambapo wanachama mbalimbali wamekuwa wakijitokeza kuwania nafasi hizo wakieleza dhamira zao za kulitumikia taifa kupitia maendeleo ya wananchi.