MJUMBE WA JUMUIYA YA WAZAZI CCM MOSHI MJINI ACHUKUA FOMU YA UBUNGE

MOSHI-KILIMANJARO.

Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Moshi Mjini, Azack Ngowi, amejiunga rasmi na mbio za kuwania ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini kwa tiketi ya chama hicho, baada ya kuchukua fomu Juni 30, 2025.

Ngowi alikabidhiwa fomu hiyo Juni 30,2025 na Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini, Frida Kaaya, katika hafla fupi iliyofanyika katika ofisi za chama zilizopo Moshi Mjini mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupokea fomu, Ngowi alisema kuwa uamuzi wake umetokana na dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi na kuendeleza misingi ya maendeleo iliyoasisiwa na CCM.

“Nikiwa kama kada wa chama, nimeamua kutumia haki yangu ya kikatiba kuomba ridhaa ya chama changu. Nikifanikiwa, nipo tayari kutoa mchango wangu kwa wananchi wa Moshi Mjini kwa moyo wa uzalendo na uwajibikaji,” alisema.

Ngowi, ambaye pia ni mfanyabiashara maarufu mjini Moshi, anawania ubunge kwa mara ya kwanza, akieleza kuwa anaamini katika siasa zenye mwelekeo wa maendeleo na mshikamano wa kijamii.

Zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu ndani ya CCM linaendelea kushika kasi katika Wilaya ya Moshi Mjini, huku wanachama kadhaa, wakiwemo wanawake, wakijitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwa kipindi kijacho.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.