YEPAO; YATOA ELIMU KWA JAMII KUPAMBANA NA MATUMIZI YA DAWA ZA KULEVYA

MOSHI-KILIMANJARO.

Tanzania, ikiwa ni miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, huungana na mataifa mengine duniani kila tarehe 26 Juni kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Matumizi na Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya. 

Lengo kuu la maadhimisho haya ni kuikumbusha jamii juu ya ukubwa wa tatizo hili na umuhimu wa kushirikiana katika kupambana nalo. huku Kauli Mbiu ya Mwaka huu inasema kuwa "Wekeza Kwenye Kinga na Tiba"

Mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanahitaji mikakati jumuishi, ikiwemo tiba kwa waathirika, ni muhimu waraibu wa dawa hizo wapate huduma stahiki zinazothibitishwa kitaalamu (evidence-based practices), pamoja na huduma endelevu kama ushauri nasaha na stadi za maisha, ili kuwasaidia wasirudi tena kwenye matumizi.

Makala haya yanaangazia namna ambavyo Shirika lisilo la kiserikali la Youth Empowerment & Psychotherapy Aid Organization (YEPAO) linavyotoa elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya kwa jamii.

Elimu, Tiba na Urejesho kwa Waraibu;


Akizungumza kuelekea maadhimisho ya Juni 26, Mkurugenzi wa YEPAO, Edward Mwendamseke, alisema kuwa shirika hilo linajikita zaidi katika utoaji wa elimu ya afya ya akili, madhara ya dawa za kulevya, pamoja na huduma za matibabu.

“Tumekuwa tukijihusisha na utoaji wa elimu ya afya ya akili, athari za dawa za kulevya, matibabu na ushauri nasaha kwa jamii, lengo letu ni kujenga jamii imara kiuchumi, kisaikolojia na kiroho,” alisema Mwendamseke.


Aliongeza kuwa mwaka 2024 pekee, YEPAO iliweza kuwahudumia waraibu 56 waliopatiwa huduma katika nyumba ya kurejesha afya na ustawi (rehabilitation center) kwa kipindi cha miezi mitatu huko KDC, ambapo walipewa pia mafunzo ya stadi za maisha ili kuwawezesha kujitegemea.

Kampeni ya Vijana na Uhamasishaji Jamii;

Kupitia mradi wa Kampeni ya Vijana, YEPAO iliendesha kampeni katika kata 12 za Manispaa ya Moshi na Moshi Vijijini, na kuwafikia watu 5,270 kwa elimu ya kuzuia matumizi ya dawa za kulevya na uhamasishaji wa kijamii.

“Mkakati huu unakwenda sambamba na juhudi za kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa vijana pamoja na kudhibiti wafanyabiashara wa dawa haramu,” alisema Mwendamseke.

Madhara ya Kijamii na Kiafya;

Mwendamseke alisema kuwa dawa za kulevya husababisha madhara makubwa ya kiafya, ikiwemo kuenea kwa virusi vya UKIMWI, homa ya ini (B na C), kifua kikuu, matatizo ya akili, pamoja na usugu wa tiba. Pia, dawa hizo husababisha matatizo ya uzazi, kama upungufu wa nguvu za kiume, kuharibika kwa mimba, na kuzaa watoto wenye matatizo ya kiafya.

Kwa upande wake, mtaalamu wa saikolojia na mnasihi, Kheri Jones Msuya, alisema kuwa tafiti zinaonesha kuwa vijana wengi wenye umri wa miaka 24 hadi 38 – walio ndani au nje ya ndoa, hutumia dawa kama bangi, mirungi, na pombe, kutokana na changamoto za maisha, mahusiano, au ukosefu wa ajira.

Ushuhuda Kutoka Kwa Mashirika Mengine;

Mkurugenzi wa Shirika la KIWAMWAKU, Ezekiel Ndembere, alisema kuwa matumizi ya dawa za kulevya yameathiri nguvu kazi ya vijana, na wengi huishia mitaani wakijihusisha na vitendo vya uhalifu ili kupata fedha za kununua dawa hizo.

“Wazazi hujikuta kwenye wakati mgumu baada ya vijana wao waliowasomesha kuishia kuwa mzigo kwa familia. Mara nyingi, huharibika kutokana na makundi wanayoshirikiana nayo,” alisema Ndembere.

Msimamo wa Serikali;

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, aliwataka vijana kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya na badala yake kushiriki shughuli halali za kiuchumi kwa ajili ya maendeleo ya familia na taifa.

“Natoa pongezi kwa YEPAO kwa kazi kubwa ya kutoa elimu na huduma ya kinga na tiba dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya,” alisema RC Babu.

Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Wenye Mahitaji Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, alisema kuwa matumizi ya dawa za kulevya yameongezeka miongoni mwa vijana, huku bangi na mirungi zikitajwa kuwa maarufu zaidi katika maeneo mengi nchini.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, alieleza kuwa serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kitaifa kupitia programu za udhibiti wa dawa za kulevya, mafunzo na matibabu kwa waathirika.

Kamishna wa Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya, Areta Lyimo, alisema kuwa vijana wengi hujiingiza katika matumizi ya dawa hizo kutokana na ushawishi wa makundi rika, baadhi ya wanafunzi huambiwa kuwa matumizi ya mirungi na bangi huwasaidia kusoma kwa muda mrefu, jambo ambalo si sahihi na huwaletea madhara makubwa baadaye.





Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.