RC KILIMANJARO AZITAKA NGO'S KUWAJIBIKA KWA JAMII


MOSHI-KILIMANJARO.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, ameyataka mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) mkoani humo kuwajibika ipasavyo kwa jamii kwa kuhakikisha kuwa mipango na miradi yao inalenga kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Akizungumza jana wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Mwaka la mashirika yasiyo ya Kiserikali kwa Mkoa wa Kilimanjaro, RC Babu alisema mashirika hayo ni mkono wa pili wa Serikali na yanapaswa kuendeshwa kwa uwazi, ufanisi na uwajibikaji.

Jukwaa hilo liliandaliwa chini ya kaulimbiu: "Tathmini ya Mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Maendeleo ya Taifa 2020/2021–2024/2025: Mafanikio, Changamoto, Fursa na Matarajio."


“Niwaombe mfanye kazi kwa bidii na kwa nia ya dhati katika kuisaidia jamii inayowazunguka. Mnapokea fedha kutoka kwa wafadhili mbalimbali kwa niaba ya Watanzania, hivyo ni muhimu kuhakikisha fedha hizo zinakwenda kutatua changamoto zao,” alisema Babu.

Alibainisha kuwa Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa mashirika hayo kutekeleza majukumu yao kwa kushirikiana na halmashauri na mikoa ili kuunga mkono jitihada za maendeleo zinazofanywa na Serikali kuu.


Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa, alisema ofisi yake itaendelea kushirikiana kwa karibu na mashirika yasiyo ya kiserikali katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhakikisha mashirika hayo yanatekeleza kwa ufanisi malengo yao.


Naye Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Msajili wa NGOs, Francisca Mwendesha, akizungumza kwa niaba ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, alisisitiza kuwa mashirika hayo yanapaswa kufuata sheria, taratibu na miongozo iliyopo katika utekelezaji wa shughuli zao.

“Mashirika lazima yaweke mbele uwajibikaji, uwazi na ufanisi katika kila hatua ya utekelezaji wa miradi yao ili kuendana na malengo ya Serikali ya kuleta maendeleo kwa wananchi,” alieleza Mwendesha.


Kwa upande wake, Mjumbe wa Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NACONGO) kwa Mkoa wa Kilimanjaro, Adam Mwamshambo, alisema baraza hilo litaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha kuwa mashirika yote yanatekeleza ipasavyo mipango yao na kutoa huduma kwa jamii katika nyanja mbalimbali zikiwemo afya, elimu, mazingira na jinsia.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.