KIWAMWAKU FOUNDATION YABADILISHA MAISHA YA VIJANA 200



MWANGA-KILIMANJARO.

Shirika lisilo la kiserikali la KIWAMWAKU Foundation limefanikiwa kuwapatia ufadhili wa kimasomo vijana zaidi ya 200 waliopo kwenye mazingira magumu katika Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, tangu mwaka 2020.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa shirika hilo, Ezekiel Dembere, alisema vijana hao wanatoka kwenye makundi yaliyo katika hatari ya kutengwa kijamii kama vile yatima, vijana waliopata daraja sifuri katika mtihani wa kidato cha nne, wanaotoka kwenye familia duni, wafanyakazi wa ndani, walioathirika na VVU pamoja na wazazi wa pekee (single mothers) wenye umri wa kati ya miaka 14 hadi 24.

“Mradi huu unajulikana kama ‘Mradi wa Kuwajengea Uwezo Vijana’ (Economic Empowerment for Group), na kila mwaka tunasaidia vijana 40 wanaotambuliwa kutoka kata 20 za Wilaya ya Mwanga,” alisema Dembere.

Akiainisha mafanikio ya mradi huo, Dembere alieleza kuwa vijana hao hupatiwa mafunzo ya elimu ya ufundi stadi yenye kujikita katika ujuzi wa vitendo kama vile ufundi mchundo, useremala, ubunifu wa mavazi, mapishi na urembo, ili kuwawezesha kujitegemea kiuchumi.

“Kwa sasa tunatekeleza mwaka wa tano wa mradi, na tumefikia idadi ya vijana 200 waliopata msaada wa moja kwa moja,” aliongeza.

Wakizungumza baadhi ya wanufaika wa mradi huo, Mwantumu Sadick Kichawele, Rajabu Athuman na Zurfa Ali, walipongeza juhudi za shirika hilo kwa kuwaibua na kuwapatia ufadhili pamoja na elimu ya vitendo.

Mwantumu Sadick Kichawele alisema, “Baada ya kuhitimu mafunzo, nimeshakuwa na sehemu yangu ya ushonaji, pia nimeajiriwa katika mgahawa wa Kifaru Restaurant, jambo ambalo limenipa uhuru wa kiuchumi.”


Naye Rajabu Athuman alisema, “Nimefungua karakana yangu ya uchomereaji vyuma ambapo ninajipatia kipato kupitia kazi hiyo, hii imeniwezesha kujitegemea na kusaidia familia yangu.”

Mbali na kusaidia vijana, shirika hilo pia linatekeleza miradi ya kuhifadhi mazingira katika shule kwa kujenga matenki ya kuvunia maji ya mvua ili kusaidia upatikanaji wa maji wakati wa kiangazi.

"Kwa mwaka 2024 pekee, matenki manane (8) yamejengwa katika shule mbalimbali katika wilaya hiyo".alisema.

Hata hivyo, Dembere alitaja changamoto ya ulipaji wa kodi ya huduma (Service Levy) inayodaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hata katika maeneo ambapo shirika linatoa msaada wa kijamii moja kwa moja, huku akieleza kuwa jambo hilo linaathiri juhudi za kufikia vijana wengi zaidi.

Akihitimisha, Dembere alitoa wito kwa mashirika mengine ya maendeleo, wadau wa sekta binafsi na serikali kushirikiana na KIWAMWAKU Foundation ili kufanikisha azma ya kuwajengea vijana mazingira bora ya kujitegemea kupitia elimu ya vitendo.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.