MOSHI-KILIMANJARO.
Wanawake wametakiwa kuunganisha nguvu ili kuimarisha malezi katika jamii kwa lengo la kujenga familia imara zitakazochangia maendeleo ya Taifa kwa miaka ijayo.Wito huo umetolewa Juni 21, 2025 na Mkuu wa wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Godfrey Mnzava, wakati wa kongamano la Wanawake mkoa wa Kilimanjaro lililofanyika jana mjini Moshi katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro.
Akizungumza kupitia taarifa iliyosomwa kwa niaba yake na Afisa Tarafa wa Kibosho, Juliana Nsanga, Mnzava alisema dunia ya sasa inakabiliwa na changamoto nyingi, zikiwemo mmomonyoko wa maadili, hali inayohitaji wanawake kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto.
“Mwanamke kama mlezi wa kwanza ana wajibu mkubwa kuhakikisha watoto wanalelewa katika misingi ya maadili mema,” alisema.
Aliongeza kuwa malezi bora ni nguzo muhimu katika familia, kwani husaidia watoto kuepuka vitendo vya kihalifu, matumizi ya dawa za kulevya na tabia nyingine hatarishi ikiwemo kuishi mitaani.
Aidha, Mnzava alieleza kuwa wanawake wana nafasi kubwa ya kuchangia pato la taifa na ukuaji wa uchumi kupitia ushiriki wao kwenye shughuli za maendeleo.
“Hatuwezi kuzungumzia maendeleo ya Taifa letu bila kutambua mchango wa wanawake, hivyo ni muhimu washirikishwe kikamilifu katika masuala ya maendeleo,” alisema.
Alifafanua kuwa kuinuka kwa hali ya kiuchumi ya mwanamke huimarisha pia ustawi wa familia kwa ujumla kwa msingi huo, serikali inaendelea kuwezesha wanawake kupitia fursa mbalimbali za mafunzo, ikiwemo ya ufundi stadi, ili waweze kupata maarifa ya kulijenga Taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TEPF, Rose Male, alisema lengo la kongamano hilo ni kutoa elimu na hamasa kwa wanawake kuhusu masuala ya malezi bora, uongozi, na uwezeshaji kiuchumi.
“Tunaamini kuwa mwanamke akipewa nafasi, elimu na ujuzi, anaweza kuwa chachu ya mabadiliko chanya na maendeleo ya familia na jamii,” alisema.
Aliongeza kuwa tafiti mbalimbali zinaonyesha familia zenye maadili na malezi bora mara nyingi huongozwa na wanawake wenye uthubutu, uvumilivu na maono.
“Semina hii imelenga kujenga msingi wa maadili mema kwa kizazi kijacho kutokana na changamoto nyingi zinazoibuka hivi sasa, zikiwemo mmomonyoko wa maadili, ukatili wa kijinsia, na ukosefu wa fursa kwa wanawake kujiendeleza kiuchumi,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Moshi Vijijini, CPA Yuvenari Shirima, alisema maendeleo ya Taifa yanategemea ustawi wa wananchi, wakiwemo wanawake na vijana, na kwamba serikali kupitia ilani ya CCM imeweka mazingira ya kuwawezesha makundi hayo kujijenga kiuchumi.
Kwa upande mwingine, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto mkoani Kilimanjaro, SP Asia Matauka, alisema vitendo vya ukatili bado ni changamoto kubwa nchini, vikihusisha wivu wa kimapenzi na mauaji ya vikongwe kutokana na imani za kishirikina.
Aliwahimiza wananchi kutoa taarifa za matukio hayo kwenye madawati ya kijinsia yaliyopo katika vituo vya polisi kote Tanzania Bara na Zanzibar.
