MAOMBI, UMOJA NDIO MSINGI WA MAFANIKIO KWENYE VITUO VYA MALEZI

                                                  

                                                          MOSHI

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini, Usharika wa Neema, limewataka walimu walezi wa watoto wadogo wanaofanya kazi katika vituo vya malezi ya mchana (Day Care) kuilinda kazi yao kwa maombi, upendo na mshikamano, kwa kuwa watoto wanakabiliwa na maadui wengi wanaotaka kuwaangamiza katika hatua zao za awali za maisha.

Kauli hiyo imetolewa na Mchungaji Daniel Mlaki wakati wa ufunguzi wa warsha ya mafunzo ya wiki mbili iliyoandaliwa na Chuo cha Mafunzo ya Walimu Montessori chini ya Usharika wa Neema, iliyowakutanisha walimu 40 kutoka mikoa ya Tanga, Arusha na Kilimanjaro.

Akizungumza katika warsha hiyo, Mchungaji Mlaki amesisitiza kuwa kazi ya kulea watoto ni huduma ya kipekee kwa Mungu, hivyo inahitaji moyo wa uvumilivu, uimara wa kiroho, nguvu za kimwili na uaminifu kwa wito wa huduma hiyo.

"Kazi mnayoifanya ni kazi ya Mungu, mnafanya kazi moja muhimu sana ya kulea watoto. Ninawasihi muimarike, msitikisike kiroho. Kazi hii inamhitaji Mungu, muwe thabiti binafsi kwa sababu inahitaji uvumilivu mkubwa," alisema Mchungaji Mlaki.

Aidha, aliwataka walimu hao kudumisha upendo kwa watoto, kwa kazi yao na kwa wenzao, akionya kuwa vituo vingi vya malezi vimekuwa vikidhoofika au kufungwa kutokana na kukosekana kwa upendo na mshikamano miongoni mwa walezi.

Warsha hiyo ni sehemu ya juhudi za Chuo cha Montessori cha Usharika wa Neema katika kuinua viwango vya malezi na elimu ya awali kwa watoto, pamoja na kuwajengea uwezo walezi wa kiroho na kitaaluma, ili waweze kushika nafasi yao muhimu katika maisha ya mtoto kabla hajaanza shule ya msingi.





Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.