WALIMU WALEZI WA VITUO VYA MALEZI YA WATOTO WADOGO WAMEHIMIZWA KUJIENDELEZA KIELIMU


                                                          MOSHI.

Walimu walezi wa watoto wadogo wanaofanya kazi katika vituo vya malezi ya mchana (day care) wametakiwa kuhakikisha wanajiendeleza kielimu ili kuongeza maarifa na ujuzi katika malezi na maendeleo ya awali ya watoto.

Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Habiba Bhou, aliyasema hayo Juni 20,205, wakati akifunga warsha ya wiki mbili iliyofanyika katika Chuo cha Mafunzo ya Montessori Ushirika wa Neema-Moshi, ambayo iliwaunganisha walimu 40 kutoka mikoa ya Tanga, Arusha na Kilimanjaro.

Warsha hiyo ililenga kuwajengea uwezo walimu walezi kwa kuwapa maarifa ya malezi bora, kuimarisha maadili ya kazi, na kuwawezesha kutengeneza na kutumia zana za kufundishia kwa njia ya vitendo, mafunzo hayo yalizingatia falsafa ya Montessori, inayomtambua mtoto kama mwenye uwezo wa kujifunza kupitia vitendo na uchunguzi wa kimazingira.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bhou alisema, “Mpango mkakati wa malezi na makuzi ya awali kwa watoto unaelekeza kuwa vituo vya kulea watoto wadogo vinapaswa kuongezwa kwenye jamii na kuendeshwa na walezi wenye weledi, hivyo ni wajibu wa kila mlezi kuhakikisha anajiendeleza kitaaluma ili kutoa huduma bora kwa watoto wetu.”

Aidha, aliipongeza serikali kwa hatua yake ya kuanzisha digrii ya malezi na makuzi ya awali, ikiwa ni hatua kubwa katika kutambua umuhimu wa taaluma hiyo ambayo hapo awali ilikuwa ikitolewa katika ngazi ya cheti na diploma pekee.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Chuo, Mariam Steven, alisema lengo kuu la warsha hiyo lilikuwa ni kuwajengea walimu uwezo wa kutumia vifaa vya kufundishia kwa njia ya vitendo, hasa kwa kuzingatia mbinu za Montessori, ili kuhakikisha watoto wanalelewa katika misingi bora inayozingatia ukuaji wa akili, hisia, jamii na kiroho.

“Mbinu hizi zinasaidia sana katika kuibua uwezo wa mtoto kujifunza kwa uhuru, kwa kuona, kushika na kushirikiana na mazingira yake,” alisema  Steven.

Mkufunzi wa Chuo, Michael Alfred, alisisitiza kuwa mfumo wa Montessori humpa mtoto uhuru wa kujifunza kupitia vitendo ambavyo humjenga kiakili na kimatendo, na kwamba mara nyingi mzazi au mlezi wa kawaida hawezi kugundua faida hizo kwa haraka.

Naye Mchungaji Daniel Mlaki wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Usharika wa Neema, aliwataka walimu kuilinda kazi yao kwa maombi, kwa kuwa watoto wana maadui wengi wanaowinda maisha yao, hasa katika hatua za awali za ukuaji.

Maliki; aliwahimiza walimu hao kuendelea kusimama katika upendo wa kweli kwa watoto, kwa kazi yao, na kwa wenzao, akisisitiza kuwa kazi ya malezi ya watoto ni huduma takatifu inayomhitaji Mungu kwa kiwango kikubwa.

Aidha, alionya kuwa vituo vingi vya malezi vinakufa kutokana na kukosekana kwa upendo miongoni mwa walimu, akiwataka walimu hao kuwa wamoja, kushirikiana na kulinda wito wao kwa bidii.

Baadhi ya washiriki wa warsha hiyo, akiwemo Florah Kweka na Florah Nkya, walielezea kuwa mbinu za kufundisha kwa njia ya vitendo zinasaidia watoto kujitegemea, kuwafanya wawe makini, na kujifunza kwa uhuru zaidi kulingana na kasi ya ukuaji wao.

Elimu ya awali imetajwa kuwa msingi wa mafanikio ya baadaye kwa mtoto, na kwa mantiki hiyo, walimu walezi wanapaswa kuwa na uelewa mpana wa maendeleo ya watoto kijamii, kihisia, kimwili na kiroho.

Falsafa ya Montessori ilianzishwa na Dkt. Maria Montessori, daktari wa afya ya akili kutoka Italia aliyezaliwa mwaka 1870 na kufariki mwaka 1952. Falsafa hiyo inasisitiza kuwa mtoto hujifunza vyema zaidi anapofanya mwenyewe kwa vitendo, badala ya kufundishwa kwa njia ya kawaida pekee.


















Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.