MWENGE WA UHURU KUTEMBELEA MIRADI 52 KILIMANJARO YENYE THAMANI YA BILIONI 84.9

MOSHI-KILIMANJARO.

Miradi  ipatayo 52, yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 84.9, iliyopo kwenye halmashauri saba za mkoa wa Kilimanjaro, inatarajiwa kutembelewa na mwenge wa Uhuru, katika ziara yake itakayoanza mkoani hapa Juni 28 hadi Julai 5, mwaka huu.


Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake jana mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, alisema kati ya miradi hiyo 20 nitawekewa mawe ya msingi, miradi mingine 23 itazinduliwa na miradi tisa itatembelewa.

Mkuu wa mkoa aliongeza kuwa kiasi cha fedha kilichotekeleza miradi hiyo kimetoka kwenye vyanzo mbali mbali ikiwemo kiasi cha bilioni 23.21 kutoka serikali kuu, bilioni 2.34 zilizotokana na halmashauri za wilaya na manispaa, bilioni 2.71 zilizotokana na nguvu za wananchi na bilioni 55.29 kutoka kwa wahisani mbali mbali.

Miradi itakayotemenelewa na mwenge mkoani hapa ni katika sekta ya afya yenye miradi nane, sekta ya miundombinu yenye miradi saba, elimu miradi 11, maji miradi saba, nishati miradi mitatu, vijana miradi saba na miradi ya kijamii tisa.

Kwa mujibu wake mkuu wa mkoa Babu, Mwenge utapokelewa katika Manispaa ya Moshi kwenye eneo la uwanja wa ndege Moshi na kukimbizwa kwenye wilaya zote kabla ya kukabidhiwa kwa mkoa wa Arusha mnamo Julai 4, katika kijiji cha Malula, kata ya Malula wilayani Arumeru.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala, alisema wao katika wilaya hiyo wamejiandaa kupokea Mwenge wa Uhuru Julai 2, ambapo utatembelea miradi mbali mbali ambayo mpaka sasa imehakikiwa kwa ajili ya uzinduzi, uwekwaji mawe ya msingi na kutembelewa.

Mwangwala, alisema kwa miaka mitano ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan wilaya ya Rombo imepokea fedha za maendeleo zaidi ya Bilioni 82, zilizoelekezwa kwenye miradi mbali mbali ya huduma kwa wananchi.

Mwenge wa Uhuru utapokelewa na viongozi wa mkoa wa Kilimanjaro, katika eneo la uwanja wa ndege wa Moshi, ukiwa umebeba ujumbe unaohamasisha wananchi kujitokeza kwenye uchaguzi mkuu wa 2025 kwa Amani na Utulivu.

Mbali na ujumbe wa kuhamasisha uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani pia Mwenge wa Uhuru umebeba ujumbe unaochagiza mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi na Ukimwi, Malaria, Dawa za Kulevya na Rushwa.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.