WAKUU WA WILAYA MKOA WA KILIMANJARO WAKABIDHIWA MAGARI MAPYA YA MILIONI 750 KWA AJILI YA KUIMARISHA UTENDAJI KAZI

MOSHI-KILIMANJARO.

Serikali kupitia Ofisi ya Rais imekabidhi magari matatu mapya kwa Wakuu wa Wilaya za Siha, Moshi Mjini na Hai, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa viongozi wa serikali katika Mkoa wa Kilimanjaro.

Magari hayo yenye thamani ya Shilingi milioni 750 ni sehemu ya vyombo vya usafiri vilivyotolewa kwa mkoa huo, kwa lengo la kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano iliyofanyika mkoani humo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha fedha hizo na kuruhusu ununuzi wa magari hayo muhimu kwa viongozi wa wilaya.

“Ninamshukuru sana Rais Samia kwa kuendelea kutuamini na kutuwezesha, magari haya yatasaidia sana katika utekelezaji wa majukumu ya viongozi wetu wa wilaya na kufikisha huduma kwa wananchi kwa ufanisi zaidi,” alisema Babu.

Babu pia aliwataka madereva wa magari hayo kuhakikisha wanayafanyia ukaguzi (service) kila baada ya kutembea kilomita 50,000 na kuwajulisha viongozi wao kabla ya ukaguzi huo kufanyika, ili kuhakikisha magari hayo yanaendelea kuwa katika hali nzuri ya kazi.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa, alisema kati ya wilaya sita za mkoa huo, wilaya tatu tayari zilikuwa na magari ya utendaji, na sasa wilaya zilizokuwa hazina zimefanikiwa kupata vitendea kazi hivyo.

“Tumekuwa tukifuatilia kwa muda, na tunamshukuru Rais kwa kutusikia, nawashukuru pia wakuu wa wilaya kwa ustahimilivu wao kwa kipindi chote walichokuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu,” alisema Nzowa.

Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa wilaya waliopokea magari hayo, Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dkt. Christopher Timbuka alisema: “Gari hili limekuja wakati muafaka, nimekuwa nikitegemea magari ya kuazima, lakini sasa nitakuwa na uwezo wa kuwafikia wananchi kwa haraka zaidi na kutatua changamoto zao kwa wakati.”

Naye Mkuu wa Wilaya ya Hai, Haasan Bomboko alisema: “Wilaya ya Hai ina vijiji 62 na vitongoji 292, kupatikana kwa gari hili kutatuwezesha kufuatilia miradi ya maendeleo, kusikiliza kero za wananchi na kufika katika maeneo yote kwa wakati.”

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava alieleza: “Tunaishukuru serikali kwa kuona umuhimu wa kuboresha mazingira ya kazi kwa viongozi na watumishi, kupitia gari hili, tutaongeza ufanisi katika kazi za kiutawala ndani ya wilaya ya Moshi.”

Makabidhiano hayo ni sehemu ya juhudi endelevu za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha watumishi na viongozi wanapata vitendea kazi bora ili kuongeza tija katika utendaji kazi wa serikali.





Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.