WANAWAKE WAJITOKEZA KUCHUKUA FOMU ZA UBUNGE MOSHI MJINI

MOSHI-KILIMANJARO.

Zoezi la uchukuaji wa fomu za kuomba ridhaa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea ubunge katika Jimbo la Moshi Mjini limeendelea kushika kasi huku wanawake wakionyesha nia ya dhati ya kushiriki katika uongozi wa juu wa kisiasa.

Miongoni mwa waliojitokeza ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Wilaya ya Moshi Mjini, Theresia Komba, ambaye amekabidhiwa rasmi fomu ya kuwania nafasi ya Ubunge wa Jimbo hilo na Katibu wa CCM Moshi Mjini Frida Kaaya, kwa tiketi ya chama hicho tawala.

Teresia, ambaye ana historia ya kushiriki kikamilifu katika siasa za ndani ya chama, aliwahi kugombea nafasi ya udiwani kupitia viti maalum mwaka 2020 na Mwaka 2022, aliwania nafasi ya Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Moshi Mjini na kufanikiwa kushinda, nafasi anayoiongoza hadi sasa.

Akizungumza baada ya kuchukua fomu hiyo, Theresia alieleza dhamira yake ya kuendeleza harakati za kuwaletea wananchi maendeleo endelevu, akisisitiza umuhimu wa kuipa nafasi sauti ya mwanamke katika ngazi ya maamuzi.

“Ni wakati wetu sasa wanawake kusimama na kuonyesha uwezo tulionao, ninaamini kwa kushirikiana na wananchi, tunaweza kuleta mabadiliko chanya Moshi Mjini,” alisema.

Zoezi la uchukuaji fomu linatarajiwa kuendelea hadi mwezi Julai 2, mwaka 2025 huku idadi ya wanawake wanaojitokeza kuchukua fomu ikitajwa kuwa ishara ya kuimarika kwa ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi nchini.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.