MOSHI-KILIMANJARO.
Aliyekuwa Diwani wa Kata ya Mawenzi katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Apaikunda Naburi, amejitokeza tena kuwania nafasi hiyo kwa kuchukua fomu ya kugombea udiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Naburi alichukua fomu hiyo Juni 29, 2025 katika Ofisi za CCM za Kata ya Mawenzi na kukabidhiwa na Katibu wa CCM wa kata hiyo, Joanitha John Byarushengo, majira ya saa 10:00 jioni.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu hiyo, Naburi alisema kuwa ameridhia maombi ya Wakazi wa Kata hiyo na Wana-CCM waliomtaka arejee kwenye kinyang’anyiro hicho kwa lengo la kuendeleza juhudi za maendeleo na ustawi wa wananchi wa Kata ya Mawenzi.
Naburi alianza kujihusisha na siasa mwaka 2005 kama Diwani wa Viti Maalum kabla ya kuchaguliwa kuwa Diwani wa Kata ya Mawenzi mwaka 2010 hadi 2015. Hata hivyo, katika uchaguzi wa mwaka 2015 Apaikunda Naburi, alishindwa kutetea kiti chake na nafasi hiyo ikachukuliwa na mgombea kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Hawa Mushi, aliyeshinda kiti hicho na baadaye mwaka 2018 Mhe; Hawa Mushi, alifariki dunia.
Baada ya kifo cha Diwani Hawa Mushi, uchaguzi mdogo ulifanyika ambapo wagombea saba waliwania nafasi hiyo, katika uchaguzi huo, Naburi aliibuka mshindi dhidi ya wapinzani wake wanaume wakiwemo Selamani Amani, Alfan Kiwango na Edward Mangesho.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, Naburi alijitosa tena na kuchukua fomu pamoja na wagombea wengine watano, akiwa Mwanamke pekee katika kinyang'anyiro hicho. alifanikiwa kushinda tena dhidi ya wapinzani wake waliokuwa miongoni mwa waliogombea pia mwaka 2018.
Hatua ya Naburi kuchukua fomu kwa mara nyingine inaashiria nia yake ya kuendeleza uongozi ndani ya Kata hiyo, huku wadadisi wa mambo ya siasa wakiona ushindani mkali unatarajiwa hasa kutoka kwa waliowahi kugombea awali.