Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Kisangara Tours, Frida Clif Mberesero, amechukua rasmi fomu ya kuomba kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuwania nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Mwanga katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Frida alifika katika Ofisi za CCM wilayani Mwanga majira ya saa sita mchana na kukabidhiwa fomu hiyo na Katibu wa CCM Wilaya ya Mwanga, Mwadawa Maulid.
Mberesero, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya fedha na utalii, anashikilia Shahada ya Diploma ya Uhasibu na Usimamizi (Advanced Diploma in Accountants in Management – CMA), pamoja na vyeti vya Teknolojia ya Habari (IT) na Huduma za Utalii (Hospitality in Tourism).
Mbali na kuwa Mkurugenzi wa Kisangara Tours, Frida pia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Ngurudoto Mountain Lodge na muasisi wa Mwanga Marathon and Festival, hafla ambayo imekuwa jukwaa muhimu la kuhamasisha afya ya mama na mtoto, matumizi ya nishati safi ya kupikia, na utalii wa ndani.
Katika jitihada zake za kutangaza vivutio vya utalii katika wilaya ya Mwanga, Frida amekuwa mstari wa mbele katika kampeni za mazingira, ikiwemo upandaji miti katika maeneo ya hospitali za umma kwa kushirikiana na wananchi, mashirika yasiyo ya kiserikali, pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Aidha, kupitia Mwanga Marathon and Festival, Frida ameweza kuwakutanisha na kuwaunganisha wana Mwanga walioko ndani na nje ya nchi (diaspora), jambo lililosaidia kukuza mshikamano na maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika wilaya hiyo.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Frida alisema kuwa ana nia ya dhati ya kuleta mabadiliko chanya katika jimbo la Mwanga kwa kutumia uzoefu wake katika sekta ya utalii, maendeleo ya jamii, na usimamizi wa rasilimali.