PRISCUS TARIMO ACHUKUA FOMU YA KUGOMBEA UBUNGE MOSHI MJINI KWA MARA NYINGINE

MOSHI-KILIMANJARO

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini mkoani Kilimanjaro, Priscus Tarimo, amejiweka tena katika mstari wa kugombea nafasi hiyo baada ya kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Tarimo alichukua fomu hiyo Juni 29, 2025, katika ofisi za CCM Wilaya ya Moshi Mjini majira ya saa 7:15 mchana, ambapo alikabidhiwa rasmi na Katibu wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM wilayani humo, Hilary Kipingi, kwa niaba ya Katibu wa CCM Wilaya.

“Nimekuja kuchukua fomu leo, Jumapili ya Juni 29, 2025. Nitazijaza kwa kufuata taratibu na kuzirejesha kwa wakati, nimesema mengi katika kipindi cha miaka mitano, kwa sasa naomba msiniulize maswali, nimechukua fomu, nitayatekeleza yale ya chama, na mengine nitarejea nayo baada ya kukamilika kwa taratibu za chama,” alisema Tarimo alipokuwa akizungumza mbele ya waandishi wa habari waliokuwa wameweka kambi katika ofisi cha chama hicho.

Jimbo la Moshi Mjini ni miongoni mwa majimbo yaliyowahi kuwa ngome ya upinzani kwa muda mrefu tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995, kwa zaidi ya miaka 25, liliongozwa na wabunge kutoka vyama vya upinzani hadi CCM kulirejesha mwaka 2020 kupitia ushindi wa Tarimo.

Katika uchaguzi wa mwaka 2020, Tarimo aliibuka mshindi kwa kupata kura 31,169 dhidi ya mpinzani wake wa karibu Raymond Mboya wa Chadema aliyepata kura 22,555.

Hatua ya Tarimo kurejea tena kuwania nafasi hiyo inafungua ukurasa mpya wa ushindani wa kisiasa ndani ya chama hicho ambpo wako wagombe wengi wanaendelea kuchukua fomu ya kugombea jimbo hilo ndani ya CCM.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.