MWENYEKITI CCM KATA YA SOWETO AREJESHA FOMU YA UDIWANI, AWAHIMIZA UWAZI NA UWAJIBIKAJI

MOSHI-KILIMANJARO.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Soweto, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Paulo Maile, amerejesha rasmi fomu ya kuwania nafasi ya Udiwani katika Kata hiyo huku akieleza dhamira yake ya kulitumikia taifa na wananchi wa Soweto kwa uadilifu na uzalendo.

Akizungumza baada ya kurejesha fomu hiyo Juni 30 mwaka 2025 katika ofisi za CCM Kata ya Soweto, Maile alisema uamuzi wake umetokana na utekelezaji wa ilani ya chama kwa vitendo pamoja na mazingira ya kidemokrasia yaliyojengwa ndani ya CCM.

“Chama cha Mapinduzi kimeonyesha uwazi, demokrasia na uwajibikaji, baada ya kutafakari kwa kina, nimeona ninao uwezo na nia ya dhati ya kuwatumikia wananchi wa Kata ya Soweto kwa weledi na bidii,” alisema Maile.

Maile aliwahi kugombea nafasi hiyo ya udiwani mwaka 2020 ambapo aliibuka mshindi wa pili kati ya wagombea tisa waliojitokeza katika kinyang’anyiro hicho.

Zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya CCM, ikiwemo ubunge na udiwani, linaendelea kwa hamasa kubwa katika Wilaya ya Moshi Mjini huku wanachama wakijitokeza kwa wingi.

Aidha, baadhi ya wanawake wameendelea kuonyesha nia ya kugombea nafasi za juu, ikiwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Wanawake (UWT) Wilaya ya Moshi Mjini, Theresia Komba, ambaye naye amechukua fomu ya ubunge katika Jimbo la Moshi Mjini.

Kwa mujibu wa Katibu wa CCM Wilaya hiyo Frida Kaaya, alisema zoezi hilo linaonesha uhai wa chama, usawa wa kijinsia na ushindani wa kidemokrasia unaowapa nafasi wanachama wenye maono ya kuleta maendeleo kwa jamii.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.