TAKUKURU YAIPONGEZA SERIKALI KWA KUIMARISHA MIUNDOMBINU

                                 

                                      ROMBO-KILIMANJARO.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, TAKUKURU, imeipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maboresho makubwa ya miundombinu ambayo yameongeza ufanisi wa taasisi hiyo nchini.

Pongezi hizo zilitolewa Juni 19, 2025, na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Francis Chalamila, kupitia taarifa iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Neema Mwakalyelye, wakati wa uzinduzi wa jengo jipya la TAKUKURU Wilayani Rombo.

Alisema serikali imeongeza watumishi, bajeti ya taasisi na kujenga majengo mapya ya kisasa nchi nzima, hatua hizo zimeongeza morali na ari kwa watumishi wa taasisi hiyo.

Alisema katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia, TAKUKURU imejenga majengo 25 ya ofisi, ambapo 17 kati yake yamekamilik ambapo  kwa mwaka huu pekee, ujenzi wa majengo manane unaendelea.

Aidha alisema katika ngazi ya mkoa, TAKUKURU inamiliki majengo 22 kati ya 25, huku ngazi ya wilaya ikiwa na majengo 42 kati ya 111, huku Ofisi za kupanga zimepungua hadi kufikia ofisi tatu tu katika mikoa na 53.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Ikulu, Mululi Mahendeka, kupitia taarifa iliyosomwa na Neema Jamu, alisifu usimamizi mzuri wa mradi huo na kusema kuwa mradi huo umeonesha jinsi TAKUKURU inavyojisimamia vizuri na kuhakikisha fedha za umma zinatumika ipasavyo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala, alisema serikali kuu imeiletea fedha zaidi ya Shilingi bilioni 80 kwa miradi ya maendeleo wilayani humo, hivyo uwepo wa jengo hilo la TAKUKURU utasaidia kusimamia matumizi yake ipasavyo.

Awali akizungumza Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kilimanjaro, Musa Chaulo, alisema tangu kuanzishwa kwa ofisi ya Rombo mwaka 2002, taasisi hiyo ilikuwa ikifanya kazi kwenye jengo la kupanga hali hiyo ilikwamisha utendaji na kuwanyima wananchi uhuru wa kufika kutoa taarifa.




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.