BARAZA LA SIHA LAAGA KWA TUZO: MKUU WA MKOA, DC NA MKURUGENZI WAPEWA HESHIMA

                                       SIHA-KILIMANJARO.

Baraza la Halmashauri ya Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro limetoa tuzo ya heshima kwa viongozi watatu waliotoa ushirikiano mkubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, hali iliyochangia mafanikio makubwa ya halmashauri hiyo hususan katika ukusanyaji wa mapato.

Tuzo hizo zilikabidhiwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Siha, Duncan Urassa, wakati wa hafla maalum iliyofanyika Juni 19, 2025, ambayo pia ilihusisha kuvunjwa kwa baraza la madiwani kupisha maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Urassa alisema kuwa viongozi waliotunukiwa tuzo hizo ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dkt. Christopher Timbuka, na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Dkt. Haji Mnasi.

“Moja ya mafanikio makubwa ambayo halmashauri yetu imeyapata ni ongezeko la makusanyo ya mapato kutoka Shilingi bilioni 1.2 mwaka 2020 hadi kufikia zaidi ya Shilingi bilioni 3.2 mwaka huu, mafanikio haya hayawezi kufikiwa bila ushirikiano wa kweli kutoka kwa viongozi hawa,” alisema Urassa.

Aliongeza kuwa mafanikio hayo pia yamechangiwa kwa kiwango kikubwa na ushirikiano uliotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Siha, ambao umekuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya halmashauri hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Timbuka aliwataka wananchi wa Siha na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuiombea nchi amani kuelekea uchaguzi mkuu, ili shughuli za maendeleo ziendelee kufanyika kwa ufanisi bila vikwazo vyovyote.

Aidha, aliwataka wananchi kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake.

“Hatuhitaji kuwa na elimu ya hali ya juu kutambua kazi nzuri ya Rais Samia, maboresho katika sekta za afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara yanaonekana wazi, na wananchi wanaleta shukrani kila anapopita,” alisema Dkt. Timbuka.

Kwa upande wake, Dkt. Haji Mnasi, ambaye alipokea tuzo hiyo kwa niaba ya viongozi wenzake, alisema mafanikio yaliyopatikana ni matokeo ya ushirikiano mkubwa kati ya watendaji wa halmashauri na baraza la madiwani lililomaliza muda wake.

Akisoma hotuba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Kiseo Nzowa, aliwataka watendaji wa halmashauri kuendelea kusimamia utekelezaji wa maamuzi ya baraza lililovunjwa, kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni.

“Wakati huu ambao baraza limevunjwa, Mkurugenzi na timu yako mnapaswa kusimamia ipasavyo utekelezaji wa maamuzi yote yaliyopitishwa, kwa kuwa yalikuwa kwa manufaa ya wananchi na Taifa, si kwa maslahi binafsi ya madiwani,” alisema Nzowa.

Tuzo hizo zimeonekana kama ishara ya kutambua mchango wa viongozi hao katika uboreshaji wa utendaji wa halmashauri na kuhamasisha uwajibikaji kwa viongozi wengine wanaoendelea kutumikia nafasi mbalimbali za kiutendaji na kisiasa.












Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.