SIHA YAPIGA HATUA KIMAENDELEO NDANI YA MIAKA MITANO – DUNCAN URASSA

                                              SIHA-KILIMANJARO.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, Duncan Urassa, ameeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kuanzia mwaka 2020 hadi 2025.

Akizungumza katika kikao maalum cha kuvunja Baraza la Madiwani, Urassa amesema halmashauri hiyo imepiga hatua kubwa katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

Kwa mujibu wa Urassa, mapato ya ndani ya halmashauri yameongezeka kutoka shilingi bilioni 1.2 mwaka 2020 hadi kufikia bilioni 3.2 kufikia Juni 15, 2025.

"Kwa mwaka wa fedha 2024/2025 pekee, halmashauri imekusanya kiasi cha shilingi bilioni 3.138, sawa na asilimia 121 ya lengo la makusanyo"alisema.

Katika kipindi hicho, halmashauri imepokea jumla ya shilingi bilioni 36 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, fedha hizo zimewezesha ujenzi wa shule mpya 10, matundu ya vyoo 365, vyumba vya madarasa 264, vituo vya afya vinne, zahanati sita, nyumba za watumishi pamoja na mabweni.

Vilevile, halmashauri imepokea shilingi milioni 669 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Kandashi (kata ya Karansi) na shilingi milioni 250 kwa ajili ya kituo cha afya Ormeriri.

Urassa amesema kuwa halmashauri ya Siha imeendelea kupata hati safi kwa miaka yote mitano, jambo linaloonesha uwajibikaji na usimamizi mzuri wa fedha za umma.

Ameeleza kuwa mafanikio haya yametokana na ushirikiano mzuri kati ya madiwani, Mkuu wa Wilaya, mkurugenzi wa halmashauri, wakuu wa idara pamoja na watendaji mbalimbali wa serikali.

Aidha alisema katika mwaka wa fedha 2023/2024, halmashauri ya Siha ilishika nafasi ya tatu kati ya halmashauri 184 nchini kwa utoaji bora wa taarifa, ikiwemo taarifa za maendeleo, na kupata tuzo ya heshima.

Mwenyekiti huyo amempongeza  mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Dkt. Haji Mnasi kwa uongozi mahiri na mchango wake mkubwa katika kusukuma gurudumu la maendeleo, huku akihimiza kuendelea kuchapa kazi kwa maslahi ya wananchi wa Siha.





Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.