MOSHI.
Serikali imewataka washiriki wa mafunzo ya usimamizi wa masuala ya uhamiaji kutoka taasisi za umma na binafsi kujiandaa kikamilifu kushiriki kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, endapo watakuwa na sifa za kuchagua au kuchaguliwa.
Kauli hiyo imetolewa Juni 2, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, wakati akifungua mafunzo ya siku tano katika Chuo cha Kikanda cha Uhamiaji – TRITA, kilichopo Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Mnzava amewataka washiriki hao kuwa mabalozi wa usalama kwa kutoa taarifa za wageni au watu wasiofahamika, hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu, akisema usalama ni jukumu la kila Mtanzania.
Aidha amepongeza uongozi wa chuo hicho kwa kuandaa mafunzo hayo, akibainisha kuwa mkoa wa Kilimanjaro unahitaji uangalizi wa karibu kutokana na wingi wa wageni wanaoingia kupitia mipaka ya kimataifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo hicho (ACI) Hoja Mahiba, amesema mafunzo hayo yanawapa washiriki maarifa ya sheria, kanuni na taratibu za uhamiaji, pamoja na namna bora ya kuhudumia wageni kwa weledi.
Amesema mafunzo hayo pia yanahusisha programu ya “Mjue Jirani Yako”, inayolenga kuimarisha usalama wa jamii kupitia ushirikishwaji wa wananchi.
Naye Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro (SACI) Augustino Malembo, amekumbusha kuwa wageni hawaruhusiwi kushiriki katika uchaguzi, na amewataka kuhakikisha wanazingatia taratibu zote za kisheria wanapokuwa nchini.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kufurahishwa kwao na elimu wanayokwenda kuipata, wakisema itawawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Akizungumza Mchungaji Peter Yohana, kutoka Kanisa la Free Pentecoste Church amesema “Mafunzo haya yatanisaidia kujua sheria za uhamiaji na namna ya kujaza taarifa za wageni tunaowapokea, natarajia kuwa na ufanisi zaidi kazini, na kuwasilisha taarifa sahihi kwa ajili ya usalama wa taifa letu.”
Naye Afisa Uhusiano wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZDU), Abdallah Sabour Khamis, amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka kwa taasisi yake.
“Katika chuo chetu tuna wanafunzi wa kimataifa kutoka zaidi ya mataifa 30, mafunzo haya yatanisaidia kuelewa taratibu sahihi za kupata vibali na jinsi ya kuwahudumia wanafunzi wageni kwa mujibu wa sheria,” amesema.


















